Friday 11th, October 2024
@
Dodoma.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa siku 15 kuanzia Oktoba 20, 2022 kwa kampuni ya Inter Country Contractors kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa miradi ya barabara katika kisiwa cha Ukerewe mkoani Mwanza.
Mheshimiwa Majaliwa ametoa agizo hilo leo (Alhamisi Oktoba 20, 2022) alipokutana na RAS Mwanza, Col. Dennis Mwilla ( Mkuu wa Wilaya Ukerewe), Joseph Mkundi (Mbunge Jimbo la Ukerewe), Joshua Manumbu ( M/Kiti wa Halmashauri ya Wilaya Ukerewe), Emmanuel L. Shelembi (Mkurugenzi wa Wilaya Ukerewe), viongozi wa TARURA (Wilaya, Mkoa na Taifa), Mhe. Angela Kairuki (Waziri OR- TAMISEMI) pamoja na viongozi mbalimbali wengine waliohudhuria katika kikao hicho katika Ofisi ya Waziri Mkuu Jijini Dodoma.
Kikao hiki kiliitishwa Kufuatia hoja zilizowasilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Col. Denis Mwila (Mkuu wa Wilaya Ukerewe) na Joseph Mkundi (Mbunge Jimbo la Ukerewe) wakati wa ziara ya Mhe Waziri Mkuu alipotembelea miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa sita katika shule ya sekondari Irugwa na ujenzi kituo cha Afya kisiwa cha Irugwa mnamo tarehe 17/10/2022 juu ya kuchelewa kukamilika kwa miradi ya barabara inayotekelezwa na kampuni ya INTERCOUNTY CONTRACTORS pamoja na upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa maeneo yaliyo nje ya Gridi ya Taifa.
Katika kikao hicho, baada ya maelezo ya watoa hoja na upande wa walalamikiwa, Mhe Waziri Mkuu Majaliwa amemwelekeza Mkandarasi kukamilisha kazi ya ujenzi huo ndani ya siku 15 ikiwa ni miradi ya ujenzi wa km. 2 za lami (Nakatunguru na Nkilizya) Ukerewe
Aidha, Mkandarasi huyo amepewa muda ifikapo tarehe 30/11/2022 miradi ya barabara za changarawe ziwe zimekamilika na kuanza kutoa huduma wilayani hapo.
“Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inatoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara, katika hili tumetoa kipaumbele kwa wakandarasi wazawa, tunachotegemea ni uaminifu wenu na utekelezaji wa miradi hii iwe ya viwango na mkamilishe kwa wakati”
Mheshimiwa Majaliwa amesema ni vyema Mameneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) Mikoa na Wilaya wakatekeleza majukumu yao ipasavyo ili kuhakikisha ujenzi wa barabara katika maeneo mbalimbali nchini na ukamilika kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa.
Katika hatua nyingine Mhe. Majaliwa amefafanua kuhusu suala la umeme kwa kuwa serikali ilikwishafikia muafaka wa jambo hilo na kampuni husika na maelekezo ya utekelezaji kutolewa, taarifa ya utekelezaji itakapowasilishwa, Mhe Waziri Mkuu atachukua hatua stahiki.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mheshimiwa Angellah Kairuki amesema wamepokea maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na kuahidi kufanya mapitio makubwa ya mfumo wa kiutendaji wa TARURA ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa miradi ndani ya taasisi hiyo.
Mwisho.
IMETOLEWA NA:
KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO.
WILAYA YA UKEREWE.
ALHAMISI, OKTOBA 20, 2022.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.