KITENGO CHA UFUGAJI NYUKI
UTANGULIZI
Kitengo cha ufugaji nyuki ni moja ya vitengo sita vilivyopo Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe. kitengo cha ufugaji Nyuki ndicho chenye jukumu la kusimamia na kuhakikisha mazao ya Nyuki yanazalishwa kwa tija na kuwa njia mbadala ya kuongeza kipato na kukuza uchumi kwa wananchi baada ya shughuli zitokanazo na kilimo na uvuvi ambazo ndio shughuli kuu katika visiwa hivi vya Ukerewe.
Kwa miaka mingi, shughuli ya kilimo imekuwa shughuli kuu yauzalishaji katika wilaya ya Ukerewe na Tanzania kwa ujumla, shughuli inayo ajili wastani wa asilimia 80 ya wananchi wote. Pamoja na uzalishaji wa mazao ya Nyuki kama asali na Nta, ufugaji wa Nyuki una mchango mkubwa katika uzalishaji na kufanikiwa kwa shughuli ya kilimo. Hii inatokana na mchango mkubwa wa uchavushaji unaofanywa na wadudu hawa kwa wastani wa asilimia 75 – 80 kutokana na taarifa za machapisho mbalimbali. Hivyo wilaya ya Ukerewe kwa kuona umuhimu wa wadudu hawa, imebaini kuwa ili kuboresha shughuli za kilimo pamoja na kuongeza aina tofauti ya mazao ni bora shughuli za kilimo zifanyike sambamba na ufugaji wa nyuki kwa lengo la kuinua ubora wa mazao ya kilimo, lakini pia mazao kama asali itokanayo na nyuki itatumika kama njia mbadala ya kuongeza kipato na lishe kwa watumiaji.
Mizinga ya nyuki imetundikwa katika miti kikundi cha TUMA kijiji cha Hamkoko
Mizinga ya nyuki ikiwa imetundikwa katika chanja kikundi cha TUMA Kijiji cha Hamkoko
SHUGHULI MBALIMBALI ZINAZOFANYIKA
Kuhamasisha ufugaji: shughuli kuu ya uchumi Wilaya ya Ukerewe ni Uvuvi. Shughuli nyingine ni kilimo, uhifadhi wa misitu na mifugo. Ufugaji Nyuki ulikuwa ukifanyika kwa baadhi ya kaya kwa sababu maalumu, aidha walina asali walikuwa na taratibu za kutafuta asali katika mapango na misitu ambako makundi ya Nyuki yalipatikana kwa urahisi. Ifinyu wa ardhi, kupanuka kwa shughuli za kilimo na makazi kulichangia kuhamisha na kupunguza mtawanyiko sawia wa makundi ya Nyuki katika maeneo mbalimbali wilayani. Changamoto hii na umuhimu wa mazao ya Nyuki imepelekea kitengo cha ufugaji Nyuki kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo kama shirika la EMEDO kuwa na shughuli ya kuhamasisha ufugaji wa Nyuki na hasa kwa kutumia mbinu ya inayosisitiza ufugaji wa makundi mengi katika eneo dogo ili kukabiliana na changamoto ya ufinyu wa ardhi.
Baadhi ya wanakikundi cha Nakaligata katika kijiji cha Murutanga wakikamua asali
Kuwezesha upatikanaji wa zana za ufugaji: Ufugaji Nyuki ni shughuli isiyohitaji matumizi makubwa ya nguvu na muda kama ilivyo katika shughuli za kilimo na uvuvi. Changamoto kubwa ni uwekezaji wa mwanzo hasa zana za ufugaji na ardhi. Kitengo kwa kushirikiana na wadau wengine wamerahisisha upatikanaji wa baadhi ya zana kama mizinga ya Nyuki. Kituo cha mafunzo ya Ufundi Bukongo na Kituo cha Ufundi cha walemavu pia Bukongo, hivi ni baadhi ya vituo vinavyotengeneza mizinga ya Nyuki kwa gharama nafuu na kutoa mafunzo bila malipo kwa mafundi wengine kutoka maeneo mbalimbali wilayani. Kwa wastani kata 19 kati ya kata 25 zilizopo Ukerewe kuna mafundi wa kutengeneza mizinga. Wadu wengine kama shirika la uhifadhi wa bonde wa ziwa victoria (LVEMP) na Rotary Club, wanatoa mchango mkubwa kuwezesha upatikanaji wa vifaa vya Ufugaji Nyuki.
Usafirishaji mizinga kwa wafugaji kata ya Muriti ufadhili wa mradi wa LVEMPII
Upatikanaji wa masoko: Ufugaji wa Nyuki unafanywa na wananchi katika mfumo wa vikundi na wafugaji binafsi. Wengi wao wanapatikana vijijini kuliko na ardhi na mazingira mazuri ya ufugaji. Pamoja na changamoto zingine, pia upatikanaji wa masoko ni changamoto nyingine kwao, kutokana na mazingira yanayopelekea kuminya wigo wa mawasiliano juu ya taarifa za masoko ya mazao ya Nyuki. Kitengo kwa kushirikiana na wafugaji hawa kimekuwa na wajibu wa kutafuta taarifa za masoko na kuhakikisha kwamba mazao haya yanapata wanunuzi.
Huduma za ugani: Ili ilani ya uchaguzi ya CCM iweze kutekelezwa kwa ufasaha, ni wajibu wa Kitengo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ili kuwezesha uzalishaji wa mazao ya nyuki yanayokidhi mahitaji ya chakula na biashara. Katika kufanikisha hitaji hili kitengo kinatoa na kuboresha huduma za ugani, hii ni pamoja na kuwashawishi wafugaji wajiunge katika vikundi vidogo vidogo vyenye umoja na nguvu vya ujasiliamali ili waweze kupata tija katika uzalishaji. Wilaya ya Ukerewe ina jumla ya wafugaji 62 walio katika vikundi na wafugaji binafsi.
Kikundi cha BMU Bugula wakiadhimisha siku ya utundikaji mizinga
Changamoto kubwa inayowakabili wafugaji hawa ni upungufu mkubwa wa wataalamu wa ufugaji Nyuki, hali hii hukwaza upatikanaji wa huduma ya wataalamu kwa wakati na muda muafaka. Ili changamoto hii iweze kupata ufumbuzi ni halmashauri ya wilaya kupata kibali cha kuajiri maafisa ugani upande wa Nyuki na kuwaelekeza kwenda kuishi jirani na wafugaji ikiwa ni pamoja na kuwaborehea makazi na huduma ya usafiri utakao wawezesha kuwafikia wafugaji kwa wakati.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.