Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Cde.Christopher Ngubiagai amewaasa waheshimiwa madiwani kufanya kazi kwa bidii,kuwaunganisha wananchi katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kijamii na kuchochea maendeleo ndani ya maeneo yao na Wilaya kwa ujumla.
Ametoa rai hiyo wakati akizungumza katika mkutano wa baraza la madiwani kujadili mapendekezo ya mpango na bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/2027 uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ukiongozwa na mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe.Ramadhan S.Mazige .
Cde.Ngubiagai ameongeza kuwa ni vyema mijadala ya baraza ikajikita zaidi kwenye hoja zenye suluhisho zenye kuleta mshikamano na maendeleo badala ya lawama au migawanyiko isiyo na tija.
" Baraza la madiwani ni kioo cha uongozi kwa wananchi,tukifanya kazi kwa pamoja,kwa maslahi mapana ya nchi yetu hakuna changamoto itakayokuwa kubwa kushindwa kuikabili."
Nae Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi Ukerewe Mhe.Ally Mambile amesema bajeti inabeba malengo na maono ya Halmashauri na kwamba ni mategemeo yake bajeti hiyo itajibu ilani ya chama cha mapinduzi.
Vincent Augustino Mbua ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe yeye ametoa taarifa ya mapokezi ya watumishi ajira mpya 2026 ambapo jumla yao ni 152 huku akibainisha kuwa zoezi la mapokezi limefanikiwa kwa 100% kwa watumishi wote 152 kuripoti kazini.
Akihitimisha mkutano huo Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe.Mazige amewataka wataalam kuzingatia ushauri na maoni yalioibuliwa katika mijadala mbalimbali wakati wa kujadili bajeti hiyo.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.