Akitia saini mkataba wa Afua ya Lishe katika eneo la ukumbi wa mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza leo October 28, 2022, Mkuu wa wilaya ya Ukerewe Col. Denis Mwila akishuhudiwa na Mkurugenzi wake Ndg. Emmanuel Sherembi amefanikiwa kutia saini mkataba wa utekelezaji wa Afia ya Lishe ambapo utekelezaji utahusisha wilaya hiyo iliyopo ndani ya Mkoa wa Mwanza.
Kabla ya utiaji saini wa mkataba huo, Mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima amewataka Wahe. Wakuu wa Wilaya hizo kuhakikisha wanaisoma mikataba hiyo na kuielewa ili waweze kuifanyia kazi kikamilifu kama ambavyo imekusudiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
"Nawaombeni Wahe. Wakuu wa Wilaya isomeni na kuielewa siyo kuisoma tu kwa kuwa mkiielewa mtaifanyia kazi na matokeo tutayaona ila mkiisoma tu mtaiacha hapo hapo," amesema Mhe.Malima.
"Chakula cha Lishe hakitakiwi kuwa na gharama kubwa... sasa nawaambia Wahe.Wakuu wa Wilaya nendeni mkatoe Elimu ya Lishe ....na haina haja ya kutumia maneno magumu waelewesheni wananchi kwamba lishe siyo lazima iwe mayai, nyama na samaki wambieni lishe ni mboga za majani kama matembele, kunde, maharage vyote hivyo ni lishe" amesisitiza Mhe.Malima.
Aidha, Mhe. Malima ameongeza kuwa mikataba hiyo wakati inashuka mwanzo ilikuwa kati ya Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wakuu wa Mikoa na sasa ni Mkuu wa Mkoa na Wahe. Wakuu wa Wilaya na baadaye Wakurugenzi.
Aidha, Mhe.Malima ameongeza kuwa Jambo kubwa katika mikataba ya Lishe ni Elimu juu ya Swala la lishe, kwa kuwa vitu vyote vinavyohusu Lishe vinapatikana katika mazingira ya wananchi.
"Wapeni Elimu wananchi juu ya matumizi ya vyakula hivyo ili viwaletee afya watoto wetu," amesisitiza Mhe. Malima
Katika hatua nyingine, Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt.Thomas Rutachunzibwa ameeleza kuwa mkataba huu ni wa msingi sana ukizingatia kuwa hali ya Udumavu iko juu takriban asilimia 29 katika mkoa wa Mwanza hivyo wameupokea Mkataba huo na kuahidi kuusimamia katika utekelezaji wake.
Nae Bw. Daniel Machunda Katibu Tawala Msaidizi Utawala Mkoa wa Mwanza akimuwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa huo Balandya Elikana, awali akimkaribisha Mhe.Mkuu wa Mkoa amesema kikao hicho ni kufuatia agizo la Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ifikapo Oktoba 30 Mikataba yote ya Lishe iwe imesainiwa.
Ikumbukwe kuwa, Mpango huu unalenga Afua za Lishe zinazohusu hatua zote za makuzi ya binadamu tangu mimba kutungwa na utekelezaji utafanyika kupitia mifumo ya kisekta, kuendeleza ushirikiano na ushirikishwaji wa wadau wote muhimu na kuhamasisha ushirikishwaji zaidi wa sekta binafsi katika kukabiliana na visababishi vya utapiamlo katika jamii.
Matokeo ya jumla yanayotarajiwa (Nadharia ya Mabadiliko) katika mpango huu ni “Wanawake, Wanaume, Watoto na Vijana Balehe nchini Tanzania wanakuwa na hali bora ya lishe na wanaishi wakiwa na afya njema na hivyo kuwa na uwezo wa kufanya kazi kwa tija zaidi”.
Imetolewa na.
Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini.
Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.