Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Cde.Christopher Ngubiagai amefanya ziara ya kawaida kutembelea miradi ya maendeleo yenye thamani ya jumla ya shilingi milioni 906,900,000 katika kata ya Ngoma lengo likiwa kukagua, kuona uendelevu sambamba na kutoa maelekezo yenye tija katika kuhakikisha kuwa miradi yote inakamilika kwa wakati kwa viwango vinavyokubalika.
Akizungumza na wataalam wakati wa ukaguzi huo katika shule ya msingi Hamukoko Mhe.Ngubiagai amesema serikali ya awamu ya sita imejipanga kupambana na maadui watatu ambao ni ujinga,maradhi na umaskini kwa kuendelea kuboresha miundo mbinu mbalimbali katika sekta zote ikiwemo afya na elimu.
Akisoma taarifa ya mradi Mkuu wa shule ya msingi Hamukoko Mwl. Maneno Paul amesema shule yake ilipokea shilingi milioni 221,200,000 kutoka serikali kuu kupitia program ya BOOST kwa ajili ya ujenzi wa vyumba saba vya madarasa,matundu 12 ya vyoo na ukarabati miundo mbinu chakavu.
"..unapoweza kumuondolea mtu ujinga utaliwezesha taifa kuwa na maendeleo.Ndo maana serikali inaendelea kuboresha mazingira wezeshi ya kutoa elimu.." amesema Cde.Ngubiagai
Nae diwani wa kata ya Ngoma Mhe.Mgeta Musa Nyagabona ameishukuru serikali kwa kutoa fedha hizo na kuwataka wananchi wake kubeba umiliki wa miradi yote inayotekekelezwa.
Sprian Rasil Msilange ni mwenyekiti wa kijiji cha Hamukoko amewasihi wananchi wake waendelee kulinda mazingira .
Miradi mingine iliyotembelewa ni pamoja na ujenzi wa kituo cha afya kata ya Ngoma awamu ya kwanza kwa gharama ya shilingi milioni 250 ambapo hadi sasa ujenzi umefikia 83%.Ukamilishaji wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na maabara tatu katika shule ya sekondari Mumbuga miradi inayotekekelezwa kwa shilingi milioni 105 fedha kutoka serikali kuu sambamba na ujenzi wa majengo ya shule mpya ya mkondo mmoja katika shule ya msingi Butiriti.
Akihitimisha ziara hiyo Cde.Ngubiagai ameelekeza jamii kushirikishwa kikamilifu katika miradi yote tangu mwanzo na kuitaka Halmashauri kuweka utaratibu wa kulinda mipaka ya maeneo yote ya umma.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.