Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Ukerewe Ndugu Vincent Augustino Mbua ameongoza kikao kazi cha maandalizi ya mapokezi ya wanafunzi kuanza darasa la awali, darasa la kwanza na waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza kilichohusisha Maafisa elimu kata na watendaji wa kata wote katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri.
Akizungumza katika kikao hicho Ndugu Mbua ametoa maelekezo kwa maafisa na watendaji hao kuhakikisha wanafunzi wote wanajiunga na masomo na kusiwepo sababu yoyote ya kuwazuia .
"... Hilo ni agizo la waziri wa nchi ofisi ya waziri Mkuu - TAMISEMI Mhe.Prof.Riziki S. Shemdoe tuhakikishe wanafunzi waliopangwa kwenye shule zetu wote wanajiunga na kidato cha kwanza mwanafunzi asizuiliwe kwa sababu yoyote ile hata kama hana sare za shule, simamieni zoezi la uandikishwaji kwa wanafunzi ..."
Nae Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Mhe. Ramadhan S. Mazige amewataka maafisa na watendaji hao kuyafanyia kazi na kutekeleza makubaliano ya kikao hicho huku akiwasihi kuwa mstari wa mbele katika kusimamia ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri katika maeneo yao.
Katika kikao hicho Maafisa hao wamethibitisha utoshelevu wa miundo mbinu tayari kuwapokea wanafunzi wa elimu ya awali, darasa la kwanza na kidato cha kwanza huku wakithibitisha kuendelea kwa mchakato wa uandikishaji na ukamilishaji baadhi ya miundo mbinu ambayo inatarajiwa kukamilika punde.
Nae Kaimu afisa elimu msingi Rasuli Amir Hamis amewasisitiza maafisa hao kutoa maelekezo kwa wakuu wa shule katika kusimamia ukamilifu wa miundombinu kama madawati ili watoto wote wapate mahali pa kukaa.
Kwa upande wake Afisa elimu taaluma msingi Joseph Gatahwa Max amewakumbusha maafisa hao kuzingatia mkakati wa ufundishaji ili kukuza taaluma na ufaulu wa wanafunzi hasa katika mitihani ya upimaji kwa watahiniwa.
Akiwasilisha taarifa ya hali miundombinu Afisa elimu kata ya Nansio Salome Maseta ameiomba serikali kuendelea kukarabati majengo yaliyochakaa na kumalizia maboma ili kupunguza adha ya mlundikano kwa wanafunzi.
|
|
|
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.