Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Kakurwa amefanya ziara katika Wilaya ya Ukerewe na kuzungumza na wadau wa uvuvi na mifugo katika kijiji cha Mulutilima kata ya Kakukuru ambapo amewataka wananchi wa Ukerewe kuthamini uvuvi na mifugo ili kunufaika na shughuli hizo.
"... tukifanya vizuri katika uvuvi na mifugo tutanufaika na mazao hayo kwa chakula na ajira kama wizara tunahakikisha tunasimamia vyema hali ya uvuvi ili kuleta faraja kwa wananchi hivyo ni jukumu letu Wanaukerewe kuwa walinzi wa ziwa letu..." Dkt. Bashiru.
Aidha Dkt. Bashiru amewahakikishia wadau wa uvuvi kuwa changamoto zitatatuliwa na wananchi watashirikishwa katika kufanya utafiti na wanakuwa sehemu ya maamuzi ili kuhakikisha mawazo yao yanatumika kwa ustawi wa uvuvi na mifugo Ukerewe.
Akiwasilisha matakwa ya Wananchi Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Ukerewe Ndugu Ramadhan Salum Mazige amesema wadau wanahitaji kuongezewa vizimba vya ufugaji wa samaki, kiwanda cha kuchakata mazao ya samaki pia kupata wataalam wa uvuvi katika chuo cha VETA cha Ukerewe ili kuongeza ufanisi katika suala zima la uvuvi.
David Kaligwa mkazi wa Kakukuru ameisifu serikali kwa jinsi ambavyo imeendelea kuwa karibu na wananchi wake na kuendelea kusikiliza na kupokea changamoto zinazowakabili huku akiiomba serikali kutatua changamoto hizo ili kuleta furaha kwa wananchi.
Kaimu Mkuu wa wilaya ya Ukerewe ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Magu Mhe. Jubilate Lawuo amewataka Wanaukerewe kuzingatia maelekezo ya serikali lakini pia kuwasilisha changamoto zao mahali zinapotakiwa ili kupatiwa ufafanuzi huku akisisitiza serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni sikivu na ipo kwaajili ya wananchi.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.