Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Mhe.Ramadhan Salum Mazige ameviasa vikundi vya mikopo ya 10% (4% wanawake ,4% vijana,2% watu wenye ulemavu) inayotolewa Halmashauri kuwa na ndoto ya kuendesha miradi mikubwa zaidi kwa lengo la kujiinua kiuchumi kupitia shughuli na miradi mbalimbali inayoibuliwa na wanakikundi wenyewe .
Akizungumza wakati akifungua mafunzo ya kujengea uwezo vikundi 18 vinavyotarajia kunufaika na mikopo hiyo juu ya usimamizi na matumizi bora ya fedha Mhe.Mazige amesema ni muhimu wahusika kupata elimu kabla ya kupewa mikopo ili kujenga uelewa wa pamoja ambao utawaondoa katika fikra za kuwaza miradi midogo midogo na kuwawezesha kuwaza miradi mikubwa yenye tija wakisimamiwa na wataalam wa maendeleo ya jamii.
"..mkope kwa malengo na utekelezaji usiende nje mpango ili muweze kurejesha vizuri na wengine waweze kunufaika na kufanya zoezi la rukopeshaji kuwa endelevu.."
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Ndugu Vincent Augustino Mbua amesema ataendelea kutenga fedha za mikopo hiyo kwa kufuata miongozo na maelekezo ya serikali.
Ndugu Mbua ameongeza kuwa fedha za mikopo ya 10% ni za serikali kwa manufaa ya wananchi wote huku akisisitiza fedha hizo sio za bure zinapaswa kurejeshwa na kuwataka wazingatie matumizi sahihi.
Wanchoke Nchichibela ni Mkuu wa idara ya maendeleo ya jamii Wilaya ya Ukerewe amesema mikopo hiyo haina ubaguzi bali inatolewa kwa wanaotimiza vigezo na kuwasihi wanavikundi kutoa taarifa sahihi kuepuka changamoto ya udanganyifu.
Jonas Mapesa na Siwema Malima ni miongoni mwa wanavikundi vya MASU group Kagera SIMATARANDO women group Bukongo waliopata mafunzo wanaipongeza Halmashauri kwa kuwaandalia mafunzo hayo ambayo yamewakumbusha majukumu, wajibu na haki zao katika kuhakikisha wanafanikiwa kupitia mikopo hiyo ya 10%.
|
|
|
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.