Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Ukerewe ndugu Wanchoke Chinchibela amefungua rasmi mafunzo ya siku moja juu ya mfumo wa taarifa za shule "School Information System"(SIS) yaliyohudhuriwa na Maafisa elimu kata, Wakuu wa shule za sekondari na msingi katika ukumbi wa mikutano wa Shule ya sekondari Bukongo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo Ndugu Chinchibela amewataka maafisa na walimu hao kubadilika kifikra na kuanza kutumia mfumo huo unaolenga kuongeza ufanisi shuleni ili kukidhi matakwa ya serikali.
Aidha, amewataka maafisa elimu kata kuwasimamia walimu wakuu wa shule zote kutoa mafunzo hayo kwa walimu ngazi zote ili halmashauri iweze kukidhi mahitaji ya mfumo sambamba na maelekezo ya serikali katika kurahisisha utunzaji na upatikanaji wa taarifa punde zinapohitajika.
Kwa upande wake Afisa elimu msingi wilaya ya Ukerewe Mwl. Bahati Mwaipasi amewasihi walimu hao kuwa waminifu na kutoa taarifa sahihi huku akiwataka kuuchukulia mfumo huo kwa uzito kwani ni agizo la serikali ili kuepuka hatua kali zinazoweza kuchukuliwa dhidi yao.
Akitoa mafunzo kuhusu mfumo huo Afisa elimu msingi vifaa na takwimu Daniel Edson Nalingigwa amesema mfumo wa SIS unahusika na taarifa zote za shule,za wanafunzi,walimu, miundo mbinu na kuwataka kuwa makini ili kutokuchanganya mchanganuo wanaotakiwa kujaza katika mfumo huku akiwaasa kuwa lengo la mfumo huo ni kuona uhai wa taasisi.
Evodias Mbila ni mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Nansio amewaomba walimu hao kuwasiliana ili kuendelea kukumbushana juu ya elimu hiyo kuepuka changamoto zinazoweza kukitokeza.
Mbali na mafunzo hayo ndugu Chinchibela amewataka Maafisa elimu kushirikiana na watendaji wa kata na vijiji katika kuhamasisha zoezi la uandikishaji watoto kwa elimu ya awali na msingi ili kukidhi maoteo na matarajio ya halmashauri kwa mwaka 2026.
|
|
|
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.