Shirika la AMREF, MAPERECE na Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Idara ya Maendeleo Ya Jamii imetoa Elimu kwa wananchi wa kata ya Murutunguru Eneo la Bugorola na Kata ya Kakukuru, lengo likiwa ni kutoa Elimu ya Ugonjwa wa Fistula.
Dkt Magdalena Dhalla Afisa Mradi Msaidizi AMREF ameeleza kuwa ugonjwa wa Fistula upo na dalili zake ni mwanamke kutokwa na mkojo au haja kubwa au vyote kwa pamoja kupitia njia ya uzazi bila kujizuia.
“Fistula ya uzazi husababishwa na uchungu wa muda mrefu kwa mama mjamzito na uzazi pingamizi bila kupata huduma ya dharura ya uzazi”.Alisema Dkt Dhalla.
Dkt Dhalla ameeleza kuwa matibabu ya Fistula ni Bure na mgonjwa hatatumia fedha yake wakati wote wa matibabu.
Nakaniwa Mshana Afisa Mfuatiliaji na Mtathimini MAPERECE amewasisitiza wanawake kuhudhuria kliniki mapema Mara tu wanapojitambua kuwa na ujauzito.
Atanasio Kwayonga Mratibu wa Haki na Sheria ametoa rai kwa wanaume kuwafikisha katika matibabu wanawake wanapopata ugonjwa huo ili kutibiwa kwa wakati.
Crispin Theobald Mratibu wa Fistula Wilaya amewasihi wanawake kuwasiliana na mabalozi wa fistula waliopo katika kata zote za Wilaya na wao wataratibu mgonjwa kufika Hospitali ya Wilaya na Hospitali ya Rufaa Bugando kwa Matibabu bila malipo yoyote.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.