"..kila mmoja hapa aone umuhimu wa lishe katika eneo lake, agenda ya lishe iwe ya kudumu katika mikusanyko yenu.Muhamasishe jamii wajue umuhimu wa kuchangia chakula shuleni.Mtoto unamzaa mwenyewe kwa nini usimpe chakula.."
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Cde.Christopher Ngubiagai wakati wa kikao cha kamati ya lishe ya wilaya hiyo kutathimini hali ya lishe kwa kipindi cha robo ya kwanza (Julai-Septemba) mwaka wa fedha 2025/2026.
Akitoa taarifa ya tathimini ya lishe kwa kipindi hicho Afisa lishe Wilaya ya Ukerewe Ndugu Ditram Kutemile amesema elimu ya lishe kwa wazazi na walezi wa watoto wa umri wa miezi 0-23 imetolewa kwa jumla ya kaya 6480 kati ya kaya 6500 katika vijiji 76 vinavyounda Halmashauri hiyo sawa na 99.7% ya kaya zote.
Aidha ameainisha mafanikio yaliyopatikana and kwa kipindi hicho kuwa uelewa wa masuala mbalimbali ya lishe umeongezeka kupitia vipindi vya redio na maeneo yenye mikusanyiko kama minada,magulio na warsha za serikali sambamba na kuongezeka kwa idadi ya shule zinazotoa huduma ya chakula shuleni kutoka shule 145 hadi shule 150 .
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo ndugu Vincent Augustino Mbua amewata watendaji kuwa watekelezaji zaidi ya kuwa wazungumzaji huku akiwasihi kuongeza nguvu katika masuala ya ukusanyaji mapato sambamba na majukumu yao ya kila siku ikiwemo usimamizi wa miradi ya maendeleo.
Allan Augustine Mhina ni Katibu tawala wa Wilaya ya Ukerewe ametoa pongezi kwa kamati hiyo huku akimuomba Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuendelea kuwajengea uwezo watendaji juu ya masuala mbalimbali ya lishe ili ujumbe ufike kwa jamii ipasavyo.
Mtendaji wa kata ya Bukiko ndugu Daymond J.Msita ameibuka kufanya vizuri katika vipengele vyote vya lishe (uchangiaji wa chakula shuleni, utekelezaji wa sheria za lishe, maadhimisho ya siku ya afya ya lishe na utoaji wa taarifa) kwa kupata alama 100% na kupongezwa na uongozi wa Wilaya hiyo kwa kazi nzuri .
Akihitimisha kikao hicho Mhe.Ngubiagai ameitaka kamati hiyo kuhakikisha masuala ya lishe yanatekelezwa kwa ubora wa juu na kuondoa kabisa hoja ya Wilaya ya Ukerewe kutokufanya vizuri.
|
|
|
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.