Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe limefanya vikao vyake vya kisheria ambapo limeketi kuanzia tarehe 11-12 juni. Baraza la Madiwani la Halmashauri linaloongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri na Diwani wa kata ya Kagunguli Mhe. George Machera Nyamaha na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri na Diwani wa Kata ya Bukindo Mhe. Gabriel Gregory Kalala pamoja na Katibu wa Baraza la madiwani na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ukerewe Bi. Ester A. Chaula. Wageni waliohudhuria baraza hilo ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Mhe. Cornel Lucas B. Magembe na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Ukerewe ndugu Ally Mambile.
Baraza la Madiwani katika siku ya kwanza ya vikao vyake limejadili taarifa mbalimbali za maendeleo zinazotekelezwa katika kata. Kata zilizowasilisha taarifa zake na kuwasilishwa katika kikao ni pamoja na kata ya Nduruma, kata ya Namilembe, kata ya Murutunguru, kata ya Muriti, kata ya Namagondo na Kata ya Ilangala.
Baraza lilipata fursa ya kupata elimu juu ya CHF iliyoboreshwa na Mratibu wa CHF Mkoa wa Mwanza Bwana Kizito Wambura. Ameeleza kuwa wilaya ya Ukerewe ni moja kati ya Halmashauri 3 zenye vifaa vya kusajilia walengwa wa mfuko wa Bima ya CHF iliyoboreshwa katika mkoa wa Mwanza. Na mpaka sasa kaya 309 ambazo zinawanufaika 1715 zimesajiliwa kwa kupata huduma hiyo. Amewaomba madiwani kusaidia kuwaelewesha wananchi kuwa kuna umuhimu wa kujiandikisha kwani watanufaika kupata matibabu kuanzia zahanati mpaka hospitali za Rufaa.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Mhe. George Nyamaha ameongoza baraza kujielekeza kujadili shughuli mbalimbali za maendeleo zilizotekelezwa katika robo ya tatu katika sekta mbalimbali kama ardhi upimaji shirikishi katika maeneo mbalimbali, ujenzi wa madarasa katika shule mbalimbali yamejengwa, afya vituo vinaendelea kuboreshwa.Baraza limeelekeza fedha zilizotolewa na serikali ikiwemo P4R zitumike kama ilivyoelekezwa na kufanya vizuri zaidi.
Aidha katika hatua nyingine Baraza la Madiwani kupitia mwenyekiti wa kamati ya Elimu Afya na Maji na diwani wa kata ya Kakerege Mhe. Sospeter Mgaya pamoja na makatibu wa vyama vya CCM na CHADEMA wamehoji kupewa sababu kwa nini maji katika vijiji vyenye miradi ya maji kutokutoka. Nae Kaimu Mhandisi wa Maji Wilaya Injinia Dartius Buchard ameeleza sababu hizo ni pamoja na kukatiwa maji kutokana na bili ya Umeme, shughuli za kibinadamu katika vyanzo vya maji na baadhi ya mabomba kuharibika. Madiwani wameagiza kuwa ufuatiliaji ufanyike kwa ukaribu kuhakikisha changamoto hizo zinafanyiwa kazi.
Baraza la madiwani limepitisha na kuridhia wajumbe 9 watakao shughulika na baraza la kata la ardhi, ambapo kata za Kagunguli na Namilembe limepata wajumbe hao ambao watakuwa na kazi katika kutatua migogoro ya ardhi katika ngazi ya kata.
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Mhe. Cornel Magembe amewataka madiwani kusimamia Halmashauri ipasavyo katika kutekeleza majukumu yake. Ameomba baraza wakati mwingine wapate wajumbe katika mabaraza ya kata ya ardhi. Amepongeza madiwani kwani maendeleo yanayofanyika katika wilaya ya Ukerewe. Amewataka watumishi wa Halmashauri kujitambua na kutekeleza bila kusukumwa na madiwani.
Magembe ameagiza Idara ya Ujenzi kujielekeza kutumia milioni 12.5 ambazo zililetwa na serikali na P4R katika elimu msingi kujenga na kukamilisha jingo zaidi ya moja na maelekezo haya yameridhiwa na madiwani wote kuwa liwe ndio azimio la baraza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ukerewe Bi. Ester A. Chaula amepokea maelekezo ya baraza na ametoa wito kwa madiwani kuendelea kushirikiana na menejimenti ilikufanikisha adhima kuu ya baraza na menejimenti ya kuwaletea wananchi maendeleo.
“Lengo kuu la chombo hiki ni kufika mbali na kuiletea wilaya ya Ukerewe maendeleo na wilaya hii tukifanikiwa vizuri wilaya yetu inauwezo wa kukusanya fedha na mapato mengi na kufikia nafasi ya tatu katika mkoa wa Mwanza” alisema Nyamaha akifunga mkutano wa Baraza la madiwani.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.