Baraza la madiwani wilaya ya Ukerewe leo limetangaza neema kwa wadau wa sekta ya uvuvi baada ya kupunguza bei za tozo kwa mazao ya samaki. Maamuzi hayo yamefanyika katika kikao cha kawaida cha madiwani kujadili taarifa za Halmashauri kwa robo ya tatu za mwaka wa fedha 2019/2020 kikao kilichofanyika katika ukumbi mkubwa wa Halmashauri.
“Katika kuhakikisha wananchi wanaondokana na makali na madhara ya ugonjwa wa virusi vya COVID 19 (corona) na wavuvi baadhi kuhamia na kufanya shughuli zao nje ya wilaya ya Ukerewe tunapendekeza bei za tozo zipungue ili kuvuta wavuvi kuvuka katika wilaya ya Ukerewe”. Alisema Mhe. Wilbard Mmbando katibu wa Madiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kasma ya ushuru wa samaki aina ya sangara, sato na dagaa pamoja na mabondo kupungua ili kuhakikisha wadau wa uvuvi wanaendelea kufanya katika katika mazingira rafiki kama hapo awali kabla ya sharia ndogo za Halmashauri ambapo bei ya kilo ya samaki aina ya sangara na sato ilikua Tsh 300, dagaa Tsh 100 na bondo Tsh 200.
Mhe George Nyamaha Mwenyekiti wa Halmashauri akatoa mapendekezo kuwa ni vema kuwa na kipindi cha mpito na matazamio wakati viwango hivyo vipya vikifanyiwa kazi ili kuhakikisha vinawezesha bajeti ya wilaya kufikiwa.
Aidha Mkurugenzi Mtandaji Ester A. Chaula ameridhia kwa maoni na mapendekezo hayo kwani kupitia maamuzi ya madiwani ambao ndio wawakilishi kwa wananchi yatakua na manufaa kwa wananchi na serikali Nae Mwanasheria wa Wilaya Mussa Mwita akalieleza baraza hilo kuwa maamuzi yoyote yatakayoamuliwa ni halali na kinachobaki ni utekelezaji tuu.
Hivyo Baraza la Madiwani katika kikao chake cha robo ya tatu kimeamua kua bei za tozo zipungue na ziwe Tsh 150 kwa kilo ya sangara na sato, Tsh 50 kwa dagaa na Tsh 2000 kwa kilo ya bondo. Tozo hizo zianze kutoza kwa kupindi cha mpito kuanzia 1/6/2020 na mwaka wa fedha 2020/2021.
Katika hatua nyingine baraza limepokea taarifa ya robo ya tatu pamoja na shughuli za maendeleo zilizofanyika kwa kipindi hiko na kuwataka wasimamizi ya miradi ya maendeleo kukamilisha miradi inayotekelezwa katika kata kukamilisha kwa wakati.
Aidha baraza limeazimia na limechukua hatua za kinidhamu kwa baadhi ya wafanyakazi ambapo watumishi wanne baraza limewafukuza kazi kutokana na tuhuma zao, wafanyakazi watatu waliokua na mashauri ya kinidhamu baraza limeamua warudishwe kazini na wapunguzwe mishahara yao, mkuu wa Kitengo mmoja amethibitishwa na wengine wawili wameongezewa muda wa matazamio, watumishi 18 wamebadilishiwa muundo, watumishi 41 wamepandishwa madaraja, watumishi watatu wamethibitishwa kazini.
Alli H. Mambile Mwenyekiti wa CCM Wilaya amepongeza baraza kwa kazi nzuri kwani wameangalia maslahi ya watu kwa kupitia upya viwango vya tozo hivyo. “usimamizi wa mapato uimarishwe na fedha ikusanywe vema kwa afya na maendeleo ya wilaya yetu” alisema Mambile.
Mhe. Cornel Magembe Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe awapongeza madiwani kwa kuonyesha uazalendo wa hali ya juu sana katika kusimamia maslahi yenu na wananchi. Amesisitiza kuwa wenye halmashauri hii ni madiwani ambao ni wawakilishi wa wananchi hivyo wawe mstari wa mbele kuhakikisha wananchi wanapata huduma kama serikali itakavyo.
Magembe amshukuru Mhe. Rais Dkt. John Magufuli kwa kuendelea kuithamini wilaya ya Ukerewe na wananchi wanyonge kwa kuendelea kuleta huduma muhimu kwao. Ameeleza mafanikio katika sekta mbali mbali ikiwemo afya, elimu na maji sekta ambazo zinawagusa wananchi moja kwa moja. “ sasa dawa zinapatikana katika vituo vya afya na zahanati, pia tenda za ambulance boti mbili zimetangazwa kwa ajili ya kisiwa cha Irugwa na Gana, meli kubwa yenye uwezo wa kubeba watu 200, gari zaidi ya 10 kwa ajili ya Ukara na itakua inatumia dakika 30 inatengenezwa na iko mbioni kukaamilika”alisema Magembe .
Makamu mwenyekiti Mhe. Gabriel G. Kalala amewashukuru wa ushirikiano anaoupata na madiwani na watumishi, na amewataka wasimamizi wa miradi wawe karibu na bei za manunuzi ziwe za bei iliopo sokoni ili fedha za force akaunti uwe na manufaa.
Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. George Nyamaha awapongeza kwa namna kila diwani alivyoshiriki katika baraza hilo na kwa kuonyesha ukomavu katika kujenga hoja kwa maslahi ya wanaukerewe. “hakika baraza hili limekua sehemu ya mabadiliko katika Wilaya hii”. Alisema Nyamaha baada ya kuongoza Baraza kupitia upya bei za tozo na kuazimia mabadiliko na yenye neema kubwa kwa wadau wa sekta ya uvuvi.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.