"..maendeleo yanapatikana sehemu yenye amani, kama hakuna amani wagonjwa msingekusanyika hapa, mpo hapa kwa ajili yakupata matibabu bila malipo ambayo yamechagizwa na serikali yetu hivyo tunahitaji kuwa na umoja na mshikamano ili kuleta utulivu ndani ya wilaya yetu na taifa kwa ujumla.." .
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Cde, Christopher Ngubiagai alipowatembelea na kuzungumza na wananchi waliokuwa wakipatiwa huduma inayoendeshwa na kambi tembezi ya matibabu bila malipo kwa ushirikiano na taasisi ya Canada African Community Health Alliance (CACHA) katika kituo cha afya Muriti kilichopo kata ya Muriti wilayani Ukerewe.
"Tumekuja kuwaona na kuwatia moyo,mtapona."
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Ukerewe ndugu Vincent Mbua amewapongeza madaktari kwa kazi nzuri wanayoendelea nayo huku akiwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo kupata huduma hizo bila malipo.
Nae daktari kiongozi wa kambi hiyo Bunhya Kayila amesema wamejipanga vizuri kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi.
Neema Mtaki mkazi wa kijiji cha Busagami yeye anakiri kuwa utolewaji wa huduma ni mzuri huku akiipongeza serikali kwa kuendelea kuwajali wananchi wake kwa kuwasogeza huduma hizo bila kuchangia gharama zozote.
Tilusasila Njobe mkazi wa kijiji cha Muriti amewaomba wananchi wenzake kuimarisha utulivu ili serikali iendelee kutoa huduma hizi bora kwa amani .
Mhe. Ngubiagai amewasihi wananchi kuwa huru kupeleka changamoto zao kwa viongozi kuanzia ngazi ya vitongoji hadi wilaya ili kupata utatuzi na kuepuka kujichukulia sheria mkononi na kufanya vurugu zinazohatarisha amani na kuzorotesha maendeleo ya jamii.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.