Mkuu wa wilaya ya Ukerewe Cde. Christopher Ngubiagai amekabidhiwa kizimba maalum cha kujikinga na wanyama hatarishi wa ziwani ikijumuisha mamba na viboko mradi unaotekelezwa na taasisi ya utafiti wa wanyamapori "Tanzania Wildlife Research Institute" (TAWIRI) ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kuimarisha usalama wa wananchi wanaotumia fukwe kwa ajili ya shughuli mbalimbali wilayani Ukerewe.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika mtaa wa Namagubo B kata ya Nansio kilipo kizimba hicho Mkuu wa Wilaya amewataka wananchi kukitunza na kukilinda kizimba hicho.
"... ni vema kukilinda kizimba hiki kama mali yetu wenyewe, tukitumie kwa usahihi, tusikiharibu tuendelee kuwa mabalozi wa usalama katika vijiji vyote vinavyopakana na ziwa..." .
Ameongeza kuwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inagusa maisha ya wananchi kwa kuhakikisha usalama wa wananchi na uendelevu wa raslimali za asili hasa kwa familia zinazoishi kandokando ya ziwa kwa kuleta vizimba hivi madhubuti.
Akitoa maelekezo kuhusu kizimba hicho Mwakilishi kutoka TAWIRI Anselm Munga amesema kizimba hicho ni sehemu salama kutumiwa kwa matumizi ya kawaida kama kufua nguo, kuchota maji kwa usalama bila kubuguziwa na wanyama hatarishi kama mamba na viboko.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya ukerewe ndugu Vincent Mbua amewasihi wananchi kufanyia shughuli zao ndani ya kizimba hicho ili kupunguza na kudhibiti ajali zinazotokea kati ya binadamu na wanyama hatarishi.
Nae afisa wanyamapori wilaya ya ukerewe ndugu Zebedayo Timotheo amewasisitiza wananchi kuendelea kutumia kizimba hicho kwa umakini zaidi ili kiweze kudumu kwa muda mrefu.
Desdelia Dastan mkazi wa Namagubo B anaishukuru serikali kwa kuwajali na kuwakumbuka wananchi wao huku akisema wataendelea kutoa elimu kwa wananchi wengine juu ya matumizi ya kizimba hicho. Akihitimisha hafla hiyo Cde. Ngubiagai amewataka wananchi wa Ukerewe kuimarisha umoja na mshikamano na kulinda amani ambayo ni tunu ya taifa letu.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.