Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Cde, Christopher Ngubiagai amekabidhiwa meli ya MV Butiama tayari kuanza kazi baada ya kusitisha safari zake kwa ajili ya matengenezo kwa takriban miezi 9 .
Akizungumza wakati akikabidhi meli hiyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya TASHICO Anselm Namala amesema meli hiyo ilipata changamoto ya mizania ya meli ,serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kujali usalama wa wananchi wake ilibidi kusitisha huduma za meli hiyo ili ifanyiwe marekebisho .
" Meli hii ilifanyiwa majaribio siku kadhaa kabla ya kuruhusiwa kuanza safari zake, nawahakikishia imekuja ikiwa bora kwa viwango vilivyohakikiwa na wataalam wetu.Ratiba ni ile ile ikitokea Mwanza asubuhi saa 3 kwenda Ukerewe na kurudi saa 8 mchana."
Cde, Ngubiagai amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha sekta ya usafiri na usafirishaji kwa kuruhusu meli ya MV Butiama kuanza kutoa huduma kwani ni fursa ya kukuza shughuli mbalimbali za kiuchumi na ni ishara ya dhamira njema kwa serikali ya awamu ya sita kwamba hakuna mwananchi atakaebaki nyuma katika masuala ya maendeleo.
"..Wana Ukerewe tunajukumu la kuitunza meli hii ,tuvae umiliki kila mmoja awe mlinzi wa mali yetu.."
Nae mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi Wilaya ya Ukerewe Mhe.Ally Khamis amesema ujio wa meli hiyo na vivuko vingine kama MV Bukondo, MV Ukerewe ni utekelezaji wa ilani ya chama cha Mapinduzi katika maboresho ya sekta ya usafiri na kusisitiza kuwa serikali ipo kazini.
Daniel Majura mkazi wa Nansio anapongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuona umuhimu wa kuboresha sekta ya usafiri kwa kuendelea kuongeza vivuko na kufanya maeneo mengi kufikika kwa urahisi.
Beatrice Bundala ni mkazi wa Kirumba Mwanza ni mfanyabiashara wa dagaa anashukuru serikali kufufua meli ya Butiama kwani sasa ana uhakika wa kuvuka asubuhi kuja Ukerewe na baadae kuvuka mchana akiwa na mzigo tayari kuingiza sokoni.
Cde, Ngubiagai amehitimisha hafla hiyo kwa kuwataka wananchi wa Ukerewe kujitokeza kwa wingi katika kampeni za uchaguzi zinazoendelea kusikiliza hoja za wagombea ili ifikakapo Oktoba 29 ,2025 wawachague viongozi wanaowataka .
|
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.