Mkuu wa wilaya ya Ukerewe Cde Christopher Ngubiagai amewaasa maafisa usafirishaji(bodaboda) kuilinda amani ya Ukerewe wakati alipohudhuria hafla ya kuunda umoja wa maafisa hao iliyofanyika katika ukumbi wa Albino uliopo kata ya Bukongo.
" Bila amani hakuna biashara, hakuna usafiri salama, kila mmoja wetu ni askari wa amani bila sare tukilinda amani tunalinda riziki zetu tunalinda usalama wetu naomba tujiepushe na migogoro na uchochezi wa aina yoyote wenye lengo la kutuvuruga..." Cde Ngubiagai.
Aidha amewataka maafisa hao kuwa na nidhamu ya fedha, heshima kwa abiria, kuwa na ushirikiano kudumisha usalama barabarani na kujiendeleza kiuchumi ili kunufaika na kazi yao.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Ukerewe Vincent Augustino Mbua amewapongeza maafisa hao kwa muungano huo wenye jumla ya wanachama 90 huku akiwasihi kuwahamasisha wengine kujiunga katika umoja huo na kuweza kujiboresha zaidi.
" Mfanye hii kazi kwa malengo ,natamani kuona mkikua kiuchumi zaidi ya hapa.Tengenezeni vikundi mje na mawazo mazuri ya kuongeza kipato chenu.Sasa kuna uvuvi wa kisasa wa kutumia vizimba njooni mpate mikopo ya asilimia 10 ."
Nae mratibu uwezeshaji wananchi kiuchumi wilaya ya Ukerewe Makungu Makungu amewashauri maafisa hao kulinda maadili ya kazi yao na kutumia fursa za mikopo ya Halmashauri.
Akihitimisha hafla hiyo mwenyekiti wa umoja wa bodaboda wilaya ya ukerewe ndugu Lazaro Kabunga amewataka maafisa hao kuulinda umoja huo huku akikiri kushirikiana nao kwa changamoto zitazojitokeza.
|
|
|
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.