"... amani siyo maneno bali ni vitendo, kila kijana awe muumini wa amani tunaweka michezo hii ili tuwe pamoja tufurahi na kushikamana kwa ajili ya Ukerewe na nchi yetu kiujumla..." Cde. Christopher Ngubiagai.
Ameyasema hayo alipohudhuria bonanza la Ukerewe one family lililowakutanisha Maafisa usafirishaji dhidi ya Machinga kwa mchezo wa soka katika uwanja wa Getrude Mongera Nansio huku Maafisa usafirishaji wakiibuka na ushindi wa bao Moja kwa sifuri.
Aidha Mhe.Ngubiagai amewataka vijana kushikamana katika nyanja zote huku akiwaahaidi kuwa serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan iko tayari kuwasikiliza vijana na kuipongeza serikali kuona umuhimu wa masuala ya vijana na kuanzisha wizara ya vijana hivyo wawe tayari kutoa mawazo yenye tija ili kuijenga Tanzania iliyo bora.
Nae Mbunge wa viti maalum kundi la vyuo vikuu Dr. Regina Malima amewataka vijana kujiepusha na maudhui yasiyofaa katika mitandao ya kijamii yanayoleta uchochezi wa vurugu huku akiwasihi vijana hao kutumia mitandao hiyo kwa faida kwa kujifunza vitu vipya na kutengeneza chaneli za biashara .
Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Ukerewe ambae pia ni afisa michezo Ndugu Yehoshefati Kalulu Foda amewapongeza vijana hao kwa mchezo mzuri na wa kiungwana waliouonyesha na akiwaomba vijana kuwa chachu ya kuinua michezo katika wilaya ya Ukerewe.
Juma Hamis Tambwe ni nahodha wa timu ya maafisa usafirishaji yeye anaipongeza serikali kwa kuendelea kuwashika mkono vijana kwa kutoa fursa za mikopo ya 10% na kuahidi kuwa wataendelea kujituma kwa manufaa yao na taifa .
P. Man ni msanii wa kizazi kipya kutoka Nansio amepongeza uongozi wa Wilaya kwa kuanzisha Bonanza hilo huku akikiri kuwa ni sehemu ambayo wasanii wamepata mahali pa kuonyesha vipaji na kutangaza kazi zao.
Mkuu huyo wa Wilaya amehitimisha kwa kutoa zawadi ya Mbuzi mwenye thamani ya shilingi laki moja kwa mshindi wa kwanza mchezo wa soka huku mshindi wa pili akijinyakulia shilingi elfu 50 na kutangaza kuwepo kwa bonanza kubwa litakalofanyika Desemba 9, 2025 kuanzia asubuhi likuhusisha michezo mbalimbali.
|
|
|
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.