"... Kwa maelezo ya wataalam wa afya matone ya Vitamin A yanaimarisha kinga ya mwili na uoni kwa watoto, dawa za minyoo zinaongeza hamu ya kula na kutibu minyoo kwa watoto niwasihi wazazi kuwaleta watoto wenu wapate chanjo hizi ili kuwalinda wasishambuliwe na magonjwa ..." DC Ngubiagai.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Ukerewe Cde.Christopher Ngubiagai alipokuwa akizindua Kampeni ya utoaji wa matone ya Vitamin "A" dawa za minyoo na upimaji wa hali ya lishe kwa watoto chini ya miaka mitano katika Kituo cha afya Nakatunguru kilichopo kata ya Nakatunguru wilayani Ukerewe .
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa wilaya ya Ukerewe Dkt. Charles Mkombe amewapongeza wazazi waliojitokeza kwa kujali afya za watoto wao huku akiwasisitiza kuwa mabalozi kwa wazazi wengine kuwaleta watoto kupata chanjo hizo.
Akisoma taarifa ya mwenendo wa zoezi la utoaji wa huduma katika mwezi wa afya na lishe ya mtoto Afisa lishe wilaya ya Ukerewe Ditram Kutemile amesema jumla ya vidonge 54,999 vya dawa za minyoo, vidonge 66,669 vya Vitamin A na tepe 350 za kupimia hali ya lishe kwa watoto vimetolewa kwa vituo 44 vya kutolea huduma za afya vilivyopo wilayani humo.
Nae Mganga Mfawidhi wa Kituo cha afya Nakatunguru Dkt. Sospeter Kanyagweta amethibitisha kuwepo kwa mwitikio mzuri kwa wazazi kuleta watoto tangu zoezi hilo lilipoanza Desemba mosi hadi hivi sasa.
Shida Msela ni mkazi wa kijiji cha Kakerege yeye anapongeza utolewaji wa huduma hizo kama chachu ya kuboresha ustawi wa afya za watoto na kujenga kizazi imara cha baadae kwa jamii ya Ukerewe.
|
|
|
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.