"... utandawazi na teknolojia ni tishio kwa utamaduni tusipokuwa makini, tuweni walinzi wa urithi wa tamaduni zetu, kwa ajili ya vizazi vijavyo, kama serikali tutaangalia uwezekano wa kuanzisha eneo la makumbusho kutunza maandiko ya waandishi wa fasihi kutoka hapa Ukerewe..."
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya Ukerewe Cde, Christopher Ngubiagai alipokuwa akifunga simpozia ya kujadili namna ya kuhifadhi na Kutafiti Lugha, Fasihi na Tamaduni za Tanzania iliyoandaliwa na Chuo cha Napoli L' Orientale (UNIOR) Italia,Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT), Shirika la utafiti (ISMEO) na Shirika la Kuboresha Mienendo na Desturi kwa Ustawi (KUMIDEU) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya wilaya ya Ukerewe.
Akiwasilisha mada ya utamaduni wa Kikerewe Mwenyekiti wa shirika la KUMIDEU Mzee Makubi Makubi amesema Ukerewe ni jamii iliyouishi ushirikiano katika nyanja zote za kijamii utamaduni ambao hadi hivi sasa unafanyika hasa katika masuala ya misiba na sherehe huku akitaja uwepo wa matambiko, ngoma za asili na utawala wa Kichifu kuwa nguzo imara zilizowaweka pamoja Wanaukerewe.
Roberto Gaudioso muadhiri kutoka chuo cha UNIOR Italia ameonyesha jinsi ambavyo fasihi iliyoandikwa na Wakerewe ilivyoimara huku akimtaja Prof. Euphrase Kezilahabi kuwa miongoni mwa wandishi wakubwa wa fasihi na kuwasihi Wanaukerewe kuendelea kuzienzi kazi zake na kuzirithisha kwa vizazi vingine.
Suzana Mgaywa ni mdau wa utamaduni Ukerewe ameiomba serikali kuwa mstari wa mbele kutangaza vivutio vya utalii katika wilaya ya Ukerewe akitaja eneo la Handebezyo lililopo Halwego na fukwe mbalimbali zilizopo Ukerewe ambavyo havipatikani kwingine zaidi ya Ukerewe.
Mbali na masuala ya kutunza utalii Mhe. Ngubiagai amewataka Wanaukerewe kutunza mazingira hasa vyanzo vya maji na kupanda miti ili kuendelea kuiweka Ukerewe salama sambamba na kuwavutia watalii na wadau wa maendeleo kuja kuwekeza kwa manufaa ya wananchi na serikali kwa ujumla.
Simpozia hiyo imetamatishwa na uwasilishwaji wa muziki wa Kikerewe kutoka Dunga Ngoma Group na Utandawazi Theatre Group (Matwi ga chalo) katika uwanja wa Getrude Mongella.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.