Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Ukerewe ndugu Vincent Augustino Mbua ameongoza timu ya menejimenti ya wilaya hiyo katika ziara ya kawaida ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo.
Akishiriki katika zoezi la uchimbaji msingi katika shule ya msingi Butiriti iliyopo kata ya Ngoma Mkurugenzi Mbua amewaasa wataalam kutekeleza miradi hiyo kwa uadilifu na weledi ili kuleta matokeo chanya kwa wananchi wa Ukerewe kwa viwango vinavyokubalika.
Miradi iliyotembelewa ni pamoja na Shule ya msingi Hamkoko iliyopo kata ya Ngoma ambapo serikali ya awamu ya sita kupitia mradi wa BOOST imetoa jumla ya shilingi milioni 221.2 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundo mbinu mbalimbali ya shule, ujenzi wa shule mpya ya mkondo mmoja ya msingi Butiriti uliopatiwa shilingi milioni 330.7, na ujenzi wa shule mpya ya msingi katika eneo la shule ya sekondari Bukanda unaotarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi milioni 330.7 , zahanati ya Chabilungo na Kituo cha afya Hamukoko .
" ..Tunawajibika kusimamia vizuri utekelezaji wa miradi hii, wahusika wote kuanzia ngazi za vitongoji hadi Wilaya kila mmoja akitimiza wajibu wake kazi ni rahisi sana na tutakamilisha kwa wakati.Tuthamini mchango wa serikali yetu inayoongozwa na Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwatendea haki wanaUkerewe .." Amesema Mbua
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.