Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Cde, Christopher Ngubiagai amewaasa wananchi wa Wilaya ya Ukerewe kulinda amani,kuhamasisha mshikamano wa kijamii na kushiriki kwa amani uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29,2025.
Ameyasema hayo wakati wa mkutano uliohusisha makundi maalum ya wazee maarufu,vijana, wanawake, viongozi wa dini,mashirika ya kiraia ,wajasiriamali,wavuvi na watumishi katika Wilaya ya Ukerewe uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya hiyo .
".. amani ni msingi wa maendeleo, bila amani hakuna uchumi, biashara au huduma bora na mshikamano hujenga nguvu ya jamii hakuna kundi dogo wala kubwa zaidi sote ni Watanzania hivyo tushirikiane kwa pamoja kujenga amani ya taifa letu kwa kushiriki kwa amani Uchaguzi mkuu wa dola.." Cde, Ngubiagai
Aidha, amewasihi wananchi kuheshimu serikali iliyopewa ridhaa ya kuongoza na kutaka kila kundi kushiriki kwa nafasi yake ili kujenga mshikamano na amani ya taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake mwenyekiti wa BAKWATA mkoa wa Mwanza Sheikh Twaha Bakari Hutari amewakumbusha viongozi wa dini kuamrisha amani na kukataza maovu huku akiwaomba viongozi wenzake kuhamasisha waumini kujitokeza kupiga kura kama sehemu ya haki yao kikatiba.
Mkurugenzi wa Shirika la msaada wa Kisheria (ULAO) Masolele Makole ameiomba kamati ya amani wilayani humo kuona namna ya kuimarisha amani na uzalendo kwa kuanzisha kambi za vijana zitakazofundisha maadili na kuisihi jamii kuwalea watoto katika mazingira ya hofu ya Mungu kuanzia ngazi ya familia kama msingi wa amani na maadili mema.
Mwakilishi wa kundi la vijana Kulwa Omari amewaomba wazazi kuwaelekeza watoto wao maana halisi ya amani na kutokuruhusu watoto wajilee maana kunasababisha mmomonyoko wa maadili na uvunjifu wa amani.
Akihitimisha mkutano huo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Ndugu Vincent Mbua ametoa shukrani kwa Wajumbe wa mkutano huo na kuwaomba wawe mabalozi wa amani na mshikamano kwa jamii.
|
|
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.