"..Watoto wanaopata chakula shuleni mara nyingi huwa na umakini mkubwa darasani lakini pia husababisha mtoto kupenda shule na kuondoa adha ya utoro na kuimarisha ukuaji mzuri wa kiakili na kihisia.."
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Cde, Christopher Ngubiagai akizungumza na wataalam wa kada mbalimbali wanaohusika na masuala ya lishe wakati wa kikao cha tathimini ya utekelezaji wa afua za lishe kwa kipindi cha Julai 1 ,2024 hadi Juni 30,2025.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa afua za lishe kwa mwaka mmoja Afisa lishe wa Wilaya ya Ukerewe Ditram Kutemile amesema jumla ya Kaya 6500 zilitembelewa na wahudumu wa afya ngazi ya jamii na kutoa unasihi wa masuala ya lishe kati ya kaya 6500 zenye watoto wa umri wa miezi 0 - 23 katika vijiji 76 sawa na asilimia 100 ya lengo.
Ditram ameainisha changamoto ambazo bado zinarudisha nyuma masuala ya upatikanaji wa chakula shuleni ikiwa ni pamoja na mwitikio hafifu wa wananchi kuchangia chakula kwa wanafunzi ambapo Halmashauri ina jumla ya shule 172 na ni shule 145 zinazotoa chakula sawa na 84.3% ya shule zinazotoa chakula huku baadhi ya shule zinazotoa chakula si wanafunzi wote wanapata chakula hicho.
Imani potofu imetajwa miongoni mwa changamoto hali inayopelekea watoto wenye utapiamlo kucheleweshwa kupeleka kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kupata matibabu stahiki.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo ndugu Vincent Augustino Mbua amesema masuala ya lishe ni kipaumbele katika Halmashauri yake hivyo atahakikisha fedha yote inayohitajika kufanikisha utekelezaji wa shughuli za lishe inatolewa kwa wakati huku akisisitiza ajenda ya lishe kuwa ya kudumu katika vikao na mikutano ya serikali za vijiji .
"Kila mmoja akitimiza wajibu wake tutapiga hatua kubwa, suala la kuendelea kuelimisha jamii halipingiki ipo siku jamii itaelewa na kubadilika na suala la utoaji chakula shuleni kuwa jambo la kawaida." amesema Ngubiagai
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.