Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la jhpiego linalojishughulisha na masuala ya afya ya mama na mtoto kupitia mradi wa "PFIZER BREAST CANCER "
wametoa semina elekezi kwa viongozi wa dini,watendaji wa kata, wahudumu wa afya ngazi ya jamii na wahanga wa saratani ya matiti juu ya ugonjwa huo na namna ya kuepukana nao.
Akifungua semina hiyo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo ndugu Chinchibera Wanchoke amesema bado jamii ya Ukerewe inahitaji kupata elimu ya kutosha juu ya saratani ya matiti kufuatia takwimu mbalimbali zitatolewa zikionyesha maeneo mengi ya ukanda wa ziwa kuwa waathirika wakuu.
Akitoa mafunzo hayo Dkt.Matobera Mugini wa hospitali ya Nansio amesema saratani ya matiti ni ugonjwa unaotokana na chembechembe hai katika matiti zinazokuwa na kugawanyika bila udhibiti maalum .
Amezitaja baadhi ya dalili za ugonjwa huo kuwa ni pamoja na uvimbe , mabadiliko ya ngozi kwenye matiti na chuchu huku akiwataka kina mama kuwahi hospitali punde wanapoona mabadiliko hayo.
Aidha Dkt.Matobera ameainisha namna ya kujilinda na saratani hiyo kwa kuwataka wanawake kujichunguza wenyewe, kuzingatia uzito sahihi wa mwili, kufanya mazoezi, kupunguza unywaji wa pombe, kuepuka matumizi ya sigara na kunyonyesha kwa kuzingatia ushauri wa wataalam wa afya.
Nae Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt.Charles Mkombe amesema wagonjwa wengi wanakwenda hospitali kwa kuchelewa hali inakuwa mbaya na kunakuwa hakuna namna ya kumsaidia mgonjwa zaidi ya kumpatia dawa za kupunguza maumivu na kumtia moyo na kuwataka kina mama kuwahi hospitali punde wanapoona mabadiliko yoyote kwenye matiti yao.
Lucas Lyimo ni Afisa takwimu na ufuatiliaji wa shirika la jhpiego yeye anasema shirika hilo lipo tayari kusaidia jamii kwa kuendelea kubuni miradi ya afya inayogusa jamii moja kwa moja na kutoa uelewa.
Akihitimisha semina hiyo Dkt.Matobera ameiasa jamii ya Ukerewe hasa kina mama ambao ndio waathirika wakuu wa saratani ya matiti kuachana na imani potofu za kishirikina juu ya ugonjwa huo na mgonjwa kujikita zaidi na matibabu ya kienyeji na baadae kwenda hospitali wakiwa wamechelewa na madhara yameshakuwa makubwa.
|
|
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.