Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imefanya ukaguzi wa ujenzi wa mradi wa maji kijiji cha Bwasa na Kigara wilayani Ukerewe, wabunge ambao ni wajumbe wa kamati hiyo wakiambatana na wataalamu kutoka TAMISEMI, wakaguzi wa hesabu za Serikali Mwanza, pamoja na Katibu Tawala wa Medkoa. Lengo kuu la ziara ya kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa ni kuona utekelezaji wa miradi ya Maendeleo inayotekelezwa na fedha za serikali katika Wilaya ya Ukerewe.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Bwasa na Kigara Mhandisi wa Maji Wilaya ya Ukerewe William Kahurananga ameeleza kuwa mradi unagharimu Tsh. 1334,610,725 na mpaka sasa kiasi cha Tsh. 1,324,610,725 zimetumika na utekelezaji wa mradi umefikia 98%. Takribani vituo vyote 20 katika vijiji viwili vinafanya kazi isipokuwa vituovinne vipya ambavyo vinafanyiwa majaribio. Mradi unatarajiwa kunufaisha wakazi 6,000 katika vijiji hivyo.
Kahurananga ameeleza baadhi ya changamoto zinazokabili mradi huo ni pamoja na kukatiwa umeme na TANESCO kutokana na kutokulipa bili, changamoto ya mfumo wa malipo , ucheleweshaji wa fedha toka hazina kuwalipa wakandarasi na kupelekea miradi kutokukamilika kwa wakati na wananchi kukosa huduma.
Ukaguzi ukiwa unaendelea wakazi wawili ambao ni Mzee Kibo Mariba na Stela Kasumbuko waliwaeleza wajumbe wa kamati kuwa wakazi wa vijiji hivyo viwili hawapati maji na wameonyesha masikitiko yao kwani maji yameanza kutoka siku moja kabla ya ziara hii. Hivyo wamewaomba viongozi kuhakikisha maji katika vijiji hivyo viwili yanapatikana.
Suala hili likaleta maswali mengi sana kutoka kwa Mwenyekiti ya Kamati Mhe. Vedastus Ngombare na wajumbe wengine kuwa ni kwanini maji hayatoki kwa muda mrefu. Ambapo mhandisi Kahurananga alieleza kuwa umeme ulikatwa na hivyo wananchi wakakosa maji. Jambo hili halikuwafurahisha wahemshimiwa wajumbe na kupelekea kutoa maazimio kama ifuatayo
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Ester Chaula ametakiwa kuzingatia sheria, na jumuiya za watumiaji maji COWSO ndizo zitumike kusimamia miradi ya maji.
Ofisi ya mkuu wa mkoa iangalie upya usanifu wa miundombinu ya vyanzo vya maji na halmashauri iweke ulinzi katika vyanzo vya maji.halmashauri isimamie na ihakikishe malipo ya TANESCO yanafanyika kwa wakati kwa kuzingatia taratibu za kifedha na sio masurufu. Na mweneyekiti wa kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa ameelekeza kuwa taarifa ya utekelezaji iwasilishwe kabla ya 1/4/2019.
naye kwa upande wake Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mwita Waitara amewataka wataalamu wa idara ya maji wilaya kuhakikisha wanawafikishia maji wananchi kwa serikali inatoa fedha kwa lengo la kuwahudumia wananchi. ameongeza kuwa kanuni na taratibu zinapaswa kuzingatiwa na kuwa COWSO jamii ya watumiaji wa maji ndizo zitumike kusimamia na sio kuunda mamlaka jambo ambalo kisheria bado halijakamilika.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.