Kamati ya Siasa ya Wilaya ikiongozwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Ukerewe Mhe. Ali Mambile imetembelea na kukagua miradi mbali mbali ya maendeleo inayotekelezwa na fedha za serikali. Miradi mine iliyotembelewa na kukaguliwa ni Ujenzi wa choo cha wanafunzi matundu 24 katika shule ya msingi Murutilima, ujenzi wa kituo cha Afya Muriti, madarasa matatu shule ya sekondari Mibungo, na mradi wa maji vijiji vya Muhula na Namagondo.
akitoa taarifa ya mradi Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Murutilima ameeleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania - (TEA). Tshs. 50,000,000.00 ilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa choo cha wanafunzi katika shule ya msingi Murutilima. Ambapo mpaka sasa kiasi cha Tsh. 45,290,000.00 kimetumika. Utekelezaji wa mradi huu ulianza tarehe 10/10/2018 na unatarajiwa kukamilika ifikapo au kabla ya tarehe 30/03/2019. Shughuli zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa msingi, boma,paa, ufitishaji wa milango na madirisha,upigaji wa lipu na sakafu na upakaji wa rangi katika jengo.
Mradi huu ukikamilika utakuwa na manufaa makubwa kwa wanafunzi wa shule ya msingi Murutilima, Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe na Taifa kwa ujumla. Utaboresha nakuongeza miundombinu muhimu ya shule na hivyo kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia. Umetengeneza ajira za muda mfupi kwa wananchi wa maeneo jirani na hivyo kuwaongezea wananchi hao kipato katika kushiriki shughuli za ujenzi. Mafundi walioshiriki katika utekelezaji wa mradi huu wameongezewa uwezo na ujuzi wa ufundi kutokana na usimamizi wa wataalam wetu wa Halmashauri.
Wajumbe wa kamati wa siasa ya wilaya wametoa mapendekezo juu ya mradi huu na wamemtaka mkurugenzi kuhakikisha maeneo yaliyosalia ukamilishwaji yanakamilishwa kwa ufasaha na wakati ili kuwezesha wanafunzi kuanza kunufaika na mradi huu, pia wameshauri elimu itolewe juu ya utumiaji mzuri wa choo hiko ili kuweza kutunza kwa manufaa ya miaka mingi ijayo.
Katika mradi wa kituo cha afya Muriti Kaimu Mganga mkuu Boniventure ameeleza kamati ya siasa kuwa Mnamo tarehe 30/06/2018 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Afya, Wazee, Jinsia na Watoto ilitoa kiasi cha Tshs. 400,000,000.00 Kwa ajili ya upanuzi wa Kituo cha Afya Muriti. Ujenzi huu ulianza kwa kazi ya kufyatua tofali tarehe 10/10/2018 baada ya kuwa tumenunua mashine ya umeme kwa kazi ya tofali, ambapo ujenzi wa majengo rasmi ulianza tarehe; 29/10/2018 na tunataraji kukamilisha kazi hiyo ifikapo tarehe 31/03/2019.
Mradi huu Umehusisha ujenzi wa majengo matano ambayo ni Jengo la Maabara, Wodi ya baba, mama na mtoto (IPD), Jengo la kuhifadhia maiti (Mortuary), Nyumba moja ya mtumishi, Jengo la Mionzi. Ujenzi umekamilika kwa asilimia 95 katika shughuli za ukamilishaji (Finishing) Hadi kufikia sasa kiasi cha fedha Tshs. 353,389,892.00 imetumika kwa ajili ya manunuzi mbalimbali ya vifaa vya ujenzi pamoja na malipo ya vibarua na mafundi.
Wajumbe wa kamati ya siasa wakiongozwa na mwenyekiti wa CCM wilaya Mhe. Ali Mambile amewataka wataalamu kufanya kazi kwa uzalendo mkubwa kwani mradi huu ukikikamilika kwa ubora uliotarajiwa utanufaisha wananchi wengi wa maeneo yanayozunguka kata ya Muriti. Mkuu wa wilaya ya Ukerewe Mhe Cornel Magembe ameelekeza kuwa mshine ya kufyatulia tofali iliyokuwa ikitumiwa katika ujenzi huo itumike katika maeneo mengine na isaidie kuongeza mapato ya halmashauri.
Ujenzi wa madarasa matatu ya shule ya sekondari Mibungo ambayo ilipokea jumla ya Tsh. 60,000,000.00 ukiwa ni ufadhiri wa MFARANSA ikiwa ni fedha ya kujenga vyumba vitatu vya madarasa. Kiasi cha Tshs. 60,000,000.00 zimetumika katika kutekeleza ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa na kutengeneza madawati 140.
Mradi huu umeleta manufaa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe na shule ya sekondari Mibungo Umeboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia. Umetengeneza ajira za muda mfupi kwa wananchi wa maeneo jirani na hivyo kuongezea kipato kwa wananchi hao. Umeongeza ari ya Wananchi kujitolea kushiriki shughuli za maendeleo kwa kuona Serikali yao ilivyowajali kwa kuleta fedha za ujenzi. Wananchi walioshiriki shughuli za ufundi wameongezewa uwezo na ujuzi wa ufundi kwa kusimamiwa na wataalam wetu wa Halmashauri.
Ujenzi wa mradi wa Maji katika vijiji vya Hamuyebe, Namagondo na Kazilankanda ulianza Mwezi Oktoba 2013 na unatarajiwa kukamilika Mwezi Juni 2019. Kazi za ujenzi wa mradi huu zinatekelezwa na Mkandarasi D4N Co LTD. Mradi huu unagharimu kiasi cha Tsh 1,632,380,960.00 na mpaka sasa kiasi cha Tsh 1,391,566,786.00 zimetumika. Utekelezaji wa mradi umefikia asilia 92. Mkandarasi yupo katika hatua za mwisho za ujenzi na kwa sasa ameanza zoezi la kufunga viungio kwenye vituo vya kuchotea maji na kufanya majaribio kwenye vituo hivyo.
Zaidi ya wakazi 8,000 katika vijijij 3 vya Hamuyebe, Namagondo na Kazilankanda watanufaika na mradi huu mara utakapokamilika. Maeneo ya mradi ambayo wananchi na taasisi hazijapata huduma ya maji vituo zaidi vitajengwa na wananchi walio tayari kuvutiwa maji ndani ya nyumba zao watapata huduma hiyo. Vilevile mradi umepeleka maji katika chuo cha Ualimu Murutunguru na shule ya sekondari Pius msekwa kupitia kijiji cha Namagondo. Mradi huu unaendeshwa na jumuiya za watumia maji (COWSO ) ambazo zimesajiliwa kisheria, zikishilikiana na watalamu ngazi ya Wilaya.
Mhandisi wa Maji Wilaya ameeleza kuwa ofisi yake inaendelea usimamizi wa karibu kwa kushirikiana na wataalamu wa mkoa ili kuhakikisha mradi unaisha kwa wakati ukiwa na ubora unaotakiwa. Kuendelea na ufuatiliaji wa karibu kwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji kwa ajili ya kupata pesa za kutekeleza mradi huu.
Ali Mambile Mwenyekiti CCM (W) amewataka Mkurugenzi kwa kushirikiana ofisi ya mhandisi kuwasimamia wakandarasi za maji katika wilaya ya Ukerewe hasa D4N kwani ameshalipwa fedha zaidi ya 80% hivyo anauwezo wa kukamilisha mradi anaongeza vibarua.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.