Serikali kupitia divisheni ya afya wilayani Ukerewe kwa kushirikiana na Canada African Community Health Alliance (CACHA) imeendelea kuwathamini wananchi wake kwa kuanzisha kambi tembezi ya matibabu bila malipo itakayofanyika kwa vituo tisa kuanzia Novemba 17 hadi 27, 2025 kwa magonjwa yote ya ndani, magonjwa ya meno, macho, Saratani ya matiti na mlango wa kizazi, huduma za watoto na akina mama sambamba na huduma za upimaji.
Akizungumuza katika ufunguzi wa kambi hiyo uliofanyika katika kituo cha afya cha Igalla kilichopo kata ya Igalla Mkuu wa wilaya ya Ukerewe Cde, Christopher Ngubiagai amewataka wananchi kuupokea mpango huo wa serikali ili kuleta ustawi wa jamii ya Ukerewe.
"... tunafahamu gharama za kupata matibabu ni kubwa sana hivyo serikali imeona ni vema kuwasogezea wananchi matibabu haya yanayo tolewa bila malipo ili tuweze kuwa na jamii yenye afya,umoja, amani, mshikamano na nguvu za kufanya kazi ili kuleta ustawi kwa wilaya yetu ya ukerewe ..." Cde Ngubiagai.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Dkt. Charles Mkombe ameipongeza serikali kwa mpango huo madhubuti wa kuwapelekea wananchi huduma huku akisema kutakuwa na ongezeko la siku saba za upasuaji katika hospitali ya Wilaya .
Nae daktari kiongozi wa kambi hiyo Bunhya Kayila amewasisitiza wananchi kuendelea kujitokeza katika vituo vyote vilivyoainishwa kwa ajili ya kupata matibabu hayo kwani timu ya madaktari ipo tayari kuwahudumia.
Maza Mlele ni mkazi wa kijiji cha Chankamba yeye amesifu jitihada za serikali kuwakumbuka wananchi wanaoishi mbali na huduma za afya za kibingwa kwa huduma hizo zinazotolewa bila malipo huku akikiri kuwa ni mkombozi kwa wananchi.
Akihitimisha ufunguzi huo Mkuu wa Wilaya amewataka wananchi wa Ukerewe kudumisha amani na utulivu ili serikali iweze kuwa huru kuleta huduma bora na maendeleo katika jamii ya Ukerewe.
|
|
|
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.