Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na mawasiliano Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe amefanya uzinduzi wa kivuko cha MV.Ukara II “HAPA KAZI TU” kitakacho safirisha abiria kati ya Bugorola na kisiwa cha Ukara katika wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza. Uzinduzi huo uliofanyika leo tarehe 19/10/2020 katika kisiwa cha Ukara na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella, Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Malima, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Mhe. Cornel Magembe na viongozi mbalimbali wa chama, Taasisi mbalimbali za Serikali na Viongozi wa dini.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe ameagiza mtendaji mkuu TEMESA kurekebisha ratiba ya meli hiyo na kuhakikisha inatoka mapema Ukara ili watu wawahi meli za kwenda Mwanza kutoka Nansio ikiwemo MV Butiama. “ TEMESA ihakikishe ratiba irekebishwe na wanaukara wawekaribu na Mwanza” alisema Kamwelwe.
“Natoa ofa meli hii ibebe abiria katika safari zake kwa siku mbili bure bila mtu kutoa nauli ili kila mwanaukara kwa siku hizi mbili afurahie huduma na meli yetu hii mpya” aliongeza Kamwelwe.
Aidha Kamwelwe amewaagiza TASAC kuendelea kutoa mafunzo kwa wamiliki, waendeshaji na watendaji mbalimbali wa vivuko ikiwemo TEMESA kwa kuzingatia taratibu na kanuni za uendeshaji wa vivuko ili kupunguza ajali za majini.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella amshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Magufuli, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi, na Mawasiliano, TEMESA na Songoro MARINE LTD kwa kujenga kivuko cha MV Ukara II “HAPA KAZI TU” ambacho kitapelekea kukua kwa uchumi wa wananchi wa Wilaya ya Ukerewe na watanzania kwa ujumla kwa kufanya usafiri na usafirishaji wa mizigo na abiria.
Akisoma taarifa fupi ya kivuko cha MV Ukara II “HAPA KAZI TU”, Mtendaji Mkuu wa TEMESA Mhandisi Japhet Masele amesema kivuko hicho kina urefu wa mita 42 na upana wa mita 10 chenye uwezo wa kubeba uzito wa tani 100 ambao ni sawa na abiria 300 na gari ndogo 10. “MV Ukara II “HAPA KAZI TU” imegharimu kiasi cha shilingi Bilioni 4.2. Alisema Masele.
Aidha Mhandisi Masele amesema Kivuko cha MV Ukara II “HAPA KAZI TU” kimefungwa vifaa vya mawasiliano ikiwemo DIRA (Compass Direction) kwa ajili ya mawasiliano. Pia amesema MV Ukara II “ HAPA KAZI TU” kina chumba maalumu kwa ajili ya wagonjwa na kimefumgwa vifaa vya uokoaji ikiwemo maboya.
Mkuu wa Wilaya wa Ukerewe Mhe. Cornel Magembe ameishukuru Serikali ya awamu wa tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli kwa kushirikiana na Wananchi wa Ukerewe baada ya ajali ya meli ya MV Nyerere iliyotokea Septemba 2018 na kuahidi kutengeneza kivuko kipya kwa ajili ya wananchi na leo Ukara imepokea kivuko cha MV Ukara II “HAPA KAZI TU”.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.