Ziara ya Mhe. Kangi Lugola tarehe 23/01/2018 Wilayani Ukerewe Kutembelea na kukagua mradi wa ufugaji wa samaki kwenye mabwawa kwa kutumia nguvu ya umeme wa jua. Mradi huo utekelezaji wake umefanyika katika kata ya Namagondo. Ziara ilianza kwa Mhe. Naibu Waziri kufika ofisi ya Mkuu wa Wilaya na kupokelewa na viongozi wa Wilaya ambapo pia alipokea Taarifa ya Wilaya.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Kangi Lugola ameutaka uongozi wa Wilaya ya Ukerewe kushirikia katika kuhakikisha Mazingira yanatunzwa kama ilivyoelekezwa katika Ilani. Amewataka pawepo na jitihada za makusudi katika kuhakikisha Miti inapandwa kwa wingi, mitaro inayopitisha majitaka inaondolewa udongo kama ilivyoelekezwa na mazingira yanatunzwa kwa ustawi wa vizazi vijavyo na kuwepo kwa hali nzuri ya hewa.
Utekelezaji wa Mradi wa Ufugaji wa samaki kwenye mabwawa kwa kutumia nishati ya jua ulianza mwezi April 2015, ukihusisha wadau mbalimbali ambao ni kikundi cha Pambazuko, shirika lisilo la kiserikali la ECOVIC ambao ndio wasimamizi wa mradi, Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Taasisi ya Utafiti ya Uvuvi na shirika la Maendeleo la UNDP ambao ndio wafadhili wa Mradi kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Ofisi ya Mak,amu wa Rais. Mradi Huo umegharimu Milioni 240,600,000 tu alisema Jackson Ndobeji pesa ambayo iliwekwa kwenye akaunti ya ECOVIC kwaajili ya shughuli za usimamizi na utunzaji wa kumbukumbu zote za fedha na kukamilisha ujenzi wa mabwawa 24 ambapo siita (6) ya SATO na (18) mumi na Kambare ambapo eneo zima la mradi ni ekari 30.
Lengo la mradi ni kutoa elimu ya ufugaji wa samaki kwenye mabwawa kupitia nishati ya jua, kutunza mazingira, upatikanaji wa lishe bora na kuondokana na umasikini, alisema Ndobeji. Pia ameainisha madhumuni yao ambapo ni pamoja na kufungua kituo cha kuzalisha kituo cha kuzalisha chakula cha samaki na kusaidia wafugaji wadogo na kuongeza mazalia ya samaki na kuongeza wastani wa kipato. Shughuli zilizofanyika ni pamoja na kuandaa eneo la mradi, mafunzo kwa wanakikundi kutembelea Misungwi na Muleba, stoo ya kutunza zana za mradi, uchimbaji wa mabwawa na uwekaji wa miundombinu na vifaa vya maji, mashine ya kusaga imefungwa na imenunuliwa, mashine ya kusukuma maji, ununuzi wa matanki ya kuzalishia vifaranga, ujenzi choo boma limekamilika na kufunikwa,wigo eneo la kufugia kwa ajili ya usalama ufyekaji wa nyasi kuzuia mmomonyoko wa udongo. Alisema Ndobeji.
Baada ya Ukaguzi wa eneo la mradi Mhe Naibu Waziri Kangi Lugola aliainisha kuwa fedha hizo zilizotolewa na Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, na kwa kutambua kuwa nchi yetu imeanza kukumbwa na mabadiliko ya tabia ya nchi, na athari kwenye kilimo, hivyo katika nchi nzima zilichaguliwa Wilaya tatu (3) ambazo ni Chamwino, Bahi na Ukerewe ambapo Ofisi ya Makamu wa Rais iliomba fedha kwa wafadhili. Mradi ulilenga kunufaisha vijiji kumi na kusaidia kilimo katika eneo hilo. Na yalitakiwa kujengwa mabwawa manne (4) ya kutotolea samaki kitu ambacho hakikufanyika na madala yake walinunua matanki manne.
Kangi alibainisha kuwa thamani halisi ya Mradi huo ni Milioni 317,400,000/= mabapo pesa hizo hazisadifu kilichofanyika badala yake inaonekana ni pesa chache ndizo zilizotumika hapo na mratibu wa mradi huo ndugu Jackson ndobeji kusema kuwa fedha zimeisha na hivyo walihitaji fedha zingine. Kangi amesikitishwa na kutokukamilika kwa mradi na amesema serikali ya Magufuli haijaribiwi bali ipo kutetea wanyonge na kupambana na mchwa wanaokula fedha za wananchi. Mratibu wa mradi alishindwa kusema ukweli juu ya thamani halisi ya mradi huo hivyo mradi kutokukamilika. “Haiwezekani mtu mmoja kusababisha madhara makubwa na kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi.” alisema Kangi.
Baada ya kubaini ubadhilifu wa fedha hizo za mradi wa samaki Namagondo kutokuwepo na kushindwa kukamilika na kushindwa kutengeneza barabara ya km.4.5 kama ilivyoainishwa kwenye mkataba, Mhe. Kangi Lugola ameagiza kukamatwa kwa Mratibu wa ECOVIC Bwana Jackson Ndobeji na ameagiza TAKUKURU na vyombo vya dola kukamatwa wote waliopo kuanzia ofisi ya makamu wa rais na wote walioko shirika la UNDP walioshirika katika ubadhilifu huo na wafikishwe mahakamani.
Kangi amemtaka Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kufuatilia kwa ukaribu miriadi yote inayotekelezwa ndani ya Wilaya hata kama mtu amejitolea thamani ya fedha zinazotumika zifahamike na pawepo uwazi na kushirikisha Halmashauri na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya. Kupitia ofisi ya Makamu wa Rais watakaa na kuona jinsi gani ya kufufua mradi huo na pesa kutokupotea bure.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.