Wananchi wa kata ya Bukiko kijiji cha Bukiko wamepatwa na maafa ya kimbunga ambapo maafa yamekumba kaya za wananchi, maeneo ya taasisi za serikali kama nyumba ya waalimu, soko la kijiji, jengo la nyumba mali ya chama cha mapinduzi(CCM). Wananchi wa Bukiko walikumbwa taharuki ya kimbunga hiko mnamo saa kumi usiku wa kuamkia tarehe 19 oktoba na kuwaacha wakiwa katika sintofahamu ya hali ambayo haikutegemewa.
Mkuu wa wilaya ya Ukerewe Mhe. Estomihn Chang’ah amewapa pole wananchi wote wa Bukiko waliopatwa na janga la kimbunga hiko. Amewataka wananchi kuwa na umoja katika kipindi hiki cha tatizo hilo na kuhifadhiana na kusaidiana pale panapohitajika kwani tatizo halina hodi. Alisema Chang’ah.
Amewataka wananchi wazingatie ujenzi bora wa miundombinu ya nyumba za kuishi kwani nyumba zikiwa imara itapunguza maafa ya uharibifu kwani hazita shambuliwa na upepo huo mkali. “Tujenge nyumba zetu katika ubora kwa kuzingatia kanuni thabiti za ujenzi ili tusikumbwe na maafa ya namna hii kwani tukiwa na nyumba imara hazitaezuliwa”. Chang’ah.
Katika kuwafariji wahanga wa kimbunga hiko Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ndugu Frank Bahati amewapa pole wote waliukumbwa na matatizo hayo na kuwataka kuwa na ushirikiano. Alieleza kuwa mtaalamu wa ujenzi ameambatana nae ili kufanya tathimini ya madhara yaliyosababishwa na upepo huo mkali na kwa miundombinu ya taasisi za serikali iliyo athirika na upepo huo zitafanyiwa marekebisho ili ziendelee kutoa huduma kwa wananchi.
Maepongeza serikali ya kata na kijiji kwa kushirikiana kikamilifu na wahanga na kuhakikisha nyumba za taasisi za serikali kama nyumba ya waalimu iliyoezuliwa na kuwaacha walimu watatu kukosa makazi na kuwahifadhi na kuanza utaratibu wa kurekebisha makazi yao ili waendelee na kazi ya ufundishaji kwa wanafunzi.
Makamo mwenyekiti wa Halmashauri Greygor Kalala alitoa pole pia kwa wahanga hao na kuwataka waepukane na tabia ya kuhusisha majanga ya kimazingira na siasa. Amewataka kuimarisha umoja wao kama wakara na wakerewe na watanzania kiujumla kwani tatizo siku zote halina hodi.
Crispin Nswasa ambaye ni Mtendaji wa kata hiyo ameeleza kuwa kaya zaidi ya ishirini (20) zimepatwa na maafa hayo pamoja na uharibifu katika paa la soko la kijiji na mashine ya kikundi. Alieleza kuwa upepo huo mkali aina ya Msoke ulianzia ziwani na kuelekea katika eneo la makazi ya watu ambapo uliambatana na mvua. Upepo huo mkali ulikua na uwezo wa kubeba paa na kulitupa umbali wa zaidi ya nusu kilometa.
Mmoja wa waathirika wa maafa hayo ambaye nyumba yake iliezuliwa ameshukuru kwa dhati serikali ya Wilaya kwa kujali na kwenda kuwapa pole. “Tunafarijika sana tukiona uongozi unajali wananchi wake hasa sisi tuliokumbwa na maafa haya na kutuacha na magofu”. Alisema Mwananchi huyo.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.