Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kupitia idara ya elimu msingi imeanza utekelezaji wa mradi wa BOOST kwa kufanya kikao na wataalam wa kada mbalimbali wanaohusika pamoja na wasimamizi wa miradi katika maeneo husika ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha kuwa fedha zote zinatumika kwa kufuata maelekezo yaliyotolewa na kutoa matokeo chanya.
Akizungumza wakati wa kikao hicho elekezi kilichokuwa na lengo la kujenga uelewa wa pamoja kwa wahusika wote juu ya namna ya kutelekeza miradi hiyo kwa ufanisi Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo ndugu Chinchibera Wanchoke ameanza kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu shilingi Bilioni 2.5 zije Ukerewe kwa ajili ya miradi ya elimu huku akieleza umuhimu kwa wananchi wa maeneo ya miradi kupata taarifa kwa usahihi ili washiriki kikamilifu kukamilisha miradi hiyo.
".. miradi hii ni ya wananchi ni lazima wajue kinachoendelea kwa usahihi ili tupate wepesi katika utekelezaj wake, tutembee katika uongozi wa kuacha alama.." amesema Chinchibera
Hassan Sizya ni mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe amewataka wataalam kusaidiana kuhakikisha kuwa maeneo yote yanayopelekewa miradi yanakuwa rafiki ki jeografia ili kupunguza gharama za mradi na kuwezesha kupata majengo mazuri ya viwango vinavyokubalika.
Nae Afisa maendeleo ya Ardhi Wilaya ya Ukerewe Ndugu Paschal Malecha amewataka wananchi wa Ukerewe kuwa tayari kupokea miradi hiyo ya maendeleo yenye manufaa kwa jamii na kuepuka migogoro ya ardhi punde mradi unapoanza kwani migogoro hiyo inachelewesha ukamilifu wa kazi .
"..Tushirikiane kila hatua,tutunze nyaraka zote kuanzia mwanzo mpaka mwisho.." amesema Kaimu Afisa elimu msingi Mwl.Matiko
Nae mkaguzi wa ndani wa Halmashauri hiyo ndugu Majura Kasika amewataka wataalam hao kuwa makini katika matumizi ya mafundi wenyeji "force account" kwa kufuata taratibu ili kuepusha hoja za kiukaguzi wakati na baada ya utekelezaji wa mradi.
Aidha wataalam hao walipata fursa ya kupata elimu ya rushwa kutoka kwa wataalam wa Taasisi ya kupinga na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Ukerewe.
Afisa Mkuu wa dawati la elimu kwa umma TAKUKURU (W)Ukerewe Erick Awael Mbise amepiga marufuku kwa wataalam kutengeneza mazingira yoyote yanayoweza kusababisha rushwa na kuwataka kuepuka matumizi mabaya ya fedha.
".. tunahitaji kuona fedha inaonyesha thamani katika miradi inayoenda kutekelezwa.." amesema Mbise
Ikumbukwe kwamba mnamo Juni 30,2025 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ilipokea jumla shilingi Bilioni 2,568,600,000 kutoka serikali kuu kupitia mradi wa BOOST kwa ajili ya ujenzi shule mpya 2, ujenzi wa vyumba vya madarasa, ujenzi wa matundu ya vyoo, ukamilishaji wa maboma sambamba ukarabati wa miundo mbinu mbalimbali ya shule za awali na msingi inayotarajiwa kukamilika Disemba 2025 .
|
|
|
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.