" Kazi ya afya ni zaidi ya ibada ,mnakumbana na changamoto nyingi za kiutumishi,za wateja mnaowahudumia lakini ni muhimu kubaki imara na kufanya kazi ndani ya maadili yenu."
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Ndugu Vincent Augustino Mbua wakati alipokuwa akizungumza na watumishi wa hospitali ya Wilaya hiyo kwa lengo la kujitambulisha kwao na kuwatia moyo katika majukumu yao kila kila siku.
Mkurugenzi Mbua amesema watumishi wa afya wamepewa dhamana kubwa na ya pekee kuwahudumia watu na kuongeza kuwa kazi hiyo ni wito na kukiri namna watumishi hao wanavyojitoa kuwahudumia wagonjwa wanaofika hospitalini hapo kupata huduma mbalimbali huku akiwataka kudumu katika maadili yao ikiwa ni pamoja na kutunza siri za wateja wao.
Kuhusu suala la ukusanyaji mapato ya hospitali Mkurugenzi huyo amemtaka Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe na wote waliopewa dhamana ya kusimamia mfumo wa GOT_HOMIS wafanye kazi ipasavyo kwa lengo la kuboresha huduma mbalimbali za kijamii na uendeshaji wa hospitali kwa ujumla.
Aidha amemtaka mfamasia wa Wilaya kuhakikisha anaweka uwiano sahihi wa msambazo wa dawa katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya ndani ya Halmashauri hiyo. ".. kikao cha leo kimetupa dira ya kuona uelekeo wetu, utaratibu mzuri sana wa kiongozi katika kazi anapotembelea watumishi wake na kuwatia moyo binafsi nampongeza sana.."Amesema Hamza Osuta mratibu wa miradi ya afya hospitali ya Wilaya ya Ukerewe.
Akihitimisha kikao hicho Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Ndugu Charles Mkombe amemshuru Mkurugenzi kwa kutenga muda na kuzungumza na watumishi wa hospitali hiyo huku akiahidi kutelekeza maelekezo yote aliyopewa kwa ubora huku akiweka wazi mpango wa Hospitali hiyo wa kuweka CCTV camera kwa baadhi ya maeneo ya kimkakati kwa ajili ya kuboresha ulinzi na usalama wa hospitali .
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.