Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Ndugu Vincent Augustino Mbua amewasisitiza watumishi wa umma kutumia mifumo elekezi ya serikali kwa ufanisi ili thamani na malengo ya uwepo wa mifumo hiyo ionekane.
Ameyasema hayo wakati akifunga mafunzo ya siku 7 kuanzia ngazi ya Wilaya juu ya mfumo wa uthibiti ubora "School Quality Assurance System" (SQAS ) yaliyotolewa kwa wataalam waandamizi,walimu wakuu wa shule za msingi,sekondari, vyuo na maafisa elimu kata.
"..serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha nyingi sana katika utengenezwaji na matumizi ya mifumo mbalimbali kwa lengo la kurahisisha kazi na kuondoa usumbufu wa kuhangaika na makaratasi,kuondoa urasimu katika shughuli mbalimbali za serikali hivyo na sisi hatuna budi kuitumia ipasavyo.."
Ameongeza kuwa uwepo wa mfumo wa PEPMIS kwa ajili ya watumishi kujaza majukumu na utekelezaji wake,mfumo wa manunuzi NeST,mfumo wa GOT_HOMIS kwenye vituo vya kutolea huduma za afya itumike ipasavyo na kukemea vikali wanaokwepa matumizi ya mifumo hiyo na kwamba usimamizi utaboreshwa ikiwa ni sehemu ya kukuza huduma bora ndani ya Ukerewe.
Nae Afisa TEHAMA wa Halmashauri hiyo, muwezeshaji mfumo wa SQAS Thobias Lupogo amewataka walimu na watumishi wote ambao ni watumiaji wa mifumo hiyo kuomba msaada mahali husika pale wanapokwama.
Mwl.Selemani Selemani ni Mkuu wa shule ya msingi Hamuyebe iliyopo kata ya Bukanda yeye anashukuru kwa mafunzo hayo huku akipongeza namna ambavyo mfumo wa SQAS unavyoonyesha uwajibikaji wa kila mtu hali itakayowawezesha walimu kujitathimini na kufanya marekebisho mwenendo wa kiutendaji haraka pale inapobidi.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.