"..Uthibiti ubora wa shule ni mchakato wa kufanya tathimini katika nyanja mbalimbali ndani ya sekta ya elimu kwa kushirikisha wadau katika kuhakikisha elimu inatolewa kwa viwango vya ubora unaokubalika.."
Rai hiyo imetolewa na mthibiti ubora wa shule Wilaya ya Ukerewe Mwl.Misana Nyasani Maige wakati akizungumza na maafisa elimu kata,wathibiti ubora wa shule wa ndani na wakuu wa shule zote zilizopo ndani ya Wilaya ya Ukerewe wakati wa mafunzo elekezi ya mfumo mpya wa "School Quality Assurance" (SQAS) ambao masuala yote ya uthibiti ubora yatafanyika kidijitali.
Mwl.Misana amezitaja na kufafanua nyanja za Uthibiti ubora wa shule ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa mtaala ambao ndani yake wanaangalia ubora wa mtaala hali kadhalika nyanja nyingine ni ubora wa ufundishaji na ujifunzaji ambao ndani yake wanaangalia mahudhurio ya walimu na wanafunzi sambamba na namna wanafunzi wanavyojifunza masuala mtambuka kama elimu ya UKIMWI.
Aidha matumizi bora ya TEHAMA yametajwa kuwa miongoni mwa nyanja za uthibiti ubora wa shule pamoja na masuala ya maadili,utamaduni na uzalendo. Victor Mtagurwa ni miongoni mwa washiriki wa semina hiyo yeye ni Makamu Mkuu wa chuo cha ualimu Murutunguru kinachopatikana ndani ya kata ya Murutunguru amesema mfumo ni mzuri,utarahisisha kazi huku akipongeza mpango wa serikali kuanzisha mfumo huo kwani ni rafiki na salama kwa utunzaji wa kumbukumbu.
".. SQAS ni mfumo mzuri taarifa yoyote ikihitajika kwa watumiaji inapatikana kwa urahisi na kwa wakati .."
Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ina jumla ya shule 174 ambapo shule za msingi ni 140 na sekondari 34.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.