Madiwani 36 waapishwa leo tarehe 4 desemba tayari kwa kuanza kazi rasmi ya kuwatumikia wananchi waliowachagua katika uchaguzi Mkuu uliofanyika oktoba 2020, zoezi la kuwaapisha madiwani limefanyika mbele ya Hakimu na kushuhudiwa na Mkuu wa Wilaya pamoja na kamati ya Ulinzi na Usalama, viongozi wa chama, na taasisi za serikali pamoja na umati wa wananchi waliofika kushuhudia tukio hilo la kihistoria kwa miaka mitano ijayo.
Madiwani wote wameapishwa ikiwa ni pamoja na wabunge wawili Mhe. Joseph Mkundi Mhe. Furaha Matondo na kwa kauli moja wamesisitiza juu ya ushirikiano kwani ndio utawezesha wilaya ya Ukerewe kuendelea zaidi.
Aidha mbali na uapishaji wa Waheshimiwa madiwani Baraza limefanya uchaguzi wa nafasi mbili ambazo ni nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ambapo matokeo kwa nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Joshua Bituro Manumbu amepata kura zote 36 sawa na 100%, nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Athanasi Malobo amepata kura 36 ambazo ni sawa na 100% ya kura zote. Hivyo Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya Josephat Mazula ambaye ndio alikua akiongoza kikao hiko cha uchaguzi amewatangaza viongozi hao.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ndugu Ali Mambile amewapongeza madiwani wote na wabunge kwa kuchaguliwa na wananchi kwa kishindo kikubwa na hii inaonyesha dhahiri kuwa mmeaminiwa na watu katika maeneo yenu. Mambile amewataka kiapo kiende sambamba na kuwatumikia wananchi kwa ueledi na uzalendo mkubwa kwa manufaa ya wilaya yetu.
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Mhe. Cornel Magembe ambaye ni mgeni mwalikwa katika kikao hiko amewapongeza sana mwenyekiti wa halmashauri na makamu wake kwa kuaminiwa kuliongoza baraza hilo kwa kipindi cha miaka mitano(5) na amewapongeza madiwani wote amewataka kwenda kusimamia maendeleo katika kata zao kwa kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa katika maeneo yao inakuwa yenye tija kwa wananchi husika na thamani ya fedha inazingatiwa. “sitegemei kuona diwani kubaki nyuma katika kutekeleza miradi ya serikali naamini mtakua mstari wa mbele kusimamia na kuhakikisha tija na ubora wa miradi ili iwanufaishe wananchi” alisema Magembe.
Katibu wa Baraza la Madiwa ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Bi. Ester A. Chaula amewapongeza sana madiwani wote kwa kula kiapo cha kuwatumikia wananchi na ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano wakati wote kama ambavyo amekua akifanya katika awamu iliyopita. “nawapongeza sana waheshimiwa madiwani wote Mwenyekiti na Makamu mwenyekiti wa halmashauri kwa kuaminiwa na chama na madiwani kuongoza jahazi hili, ofisi yangu itaendelea kutoa ushirikiano wakati wote nitakuwepo kuwatumikia” aliongeza Chaula.
Mhe Joshua Bituro Manumbu Mwenyekiti wa Halmashauri ameeleza vipaumbele vyake katika kipindi cha uongozi wake ni elimu ambayo itaenda sambamba na kumalizia maabara zote, Maji kuboresha miundombinu ya maji na upatikanaji wa maji wa uhakika, miundombinu ya barabara kuptipika katika misimu yote lakini kubwa ni kuongeza mapato ya halmashauri kwa kubuni vyanzo vipya vya mapato na kushirikiana na wananchi na wadau ili kuona namna ya kupunguza kero za tozo nyingi.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.