Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ambaye pia ni Mkuu wa divisheni ya maendeleo ya jamii ndugu Wanchoke Chinchibera amefungua rasmi mafunzo ya siku tatu kwa ajili ya maafisa maendeleo ya jamii wapya katika jukumu hilo lengo likiwa ni kujenga uelewa wa pamoja juu ya kanuni, miongozo ya uendeshaji wa zoezi la utoaji mikopo ya 10% ya Halmashauri ambapo 4% ni kwa ajili ya wanawake,4% vijana na 2% kwa ajili ya watu wenye ulemavu .
"..Ni utaratibu wa kawaida tunapokuwa na watumishi wapya kuwaelekeza namna tunavyofanya kazi ili twende pamoja katika utekelezaji mzuri wa kazi zetu.Mfahamu mnawajibika kuzitambua mila na desturi za jamii tunayoihudumia ili muwezeshe kutoa huduma stahiki na kuepuka migongano isiyokuwa ya lazima.."
Akiongoza mjadala Mratibu Uwezeshaji wa wananchi kiuchumi wilaya ya Ukererwe, ndugu Makungu S Makungu amesema ni muhimu kwa maafisa hao kujengewa uwezo katika masuala ya elimu kwa wajasiriamali na kupata ujuzi na kuongeza tija katika masuala yote yanayohusu maendeleo ya jamii.
Nae Msajili Msaidizi wa Mashirika yasiyo ya kiserikali Bi.Rhoda Ogada amewasilisha mada ya utambuzi na usajili wa wafanyabiashara wadogo wadogo (WBN) na kubainisha makundi ya Wamachinga, Mama au Baba lishe, Bodaboda, Wauza genge na wafanyabishara wengine ambao mitaji yao havuki shilingi milioni 4,000,000 kuwa wanatakiwa wajisajili ili kupata kitambulisho cha mjasiriamali kwa gharama ya Tsh. 20,000 ndani ya miaka mitatu na kutambulika na Halmashauri.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Dawati la Msaada Kisheria Bi.Janeth Lemi akiwasilisha mada ya Huduma ya utoaji wa msaada kisheria amewaomba maafisa hao kutambua migogoro mbalimbali inayoihusu jamii na kuwa na utangulizi juu ya utatuzi wa migogoro hiyo huku akiorodhesha baadhi ya kesi ambazo dawati hilo linahusika nazo ikiwemo migogoro ya mirathi, ndoa, ardhi, unyanyasaji wa kijinsia, kazi na ajira na matunzo ya mtoto kwa jamii .
Anitha Manyanya ni Afisa maendeleo ya jamii kata ya Murutunguru yeye anashukuru kupata mafunzo hayo ambayo anasema yamempatia mwanga na dira katika majukumu mapya
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.