Chuo cha ufundi stadi VETA wilaya ya Ukerewe kimefanya mahafali yake ya kwanza kikihusisha wahitimu wa kada ya ufundi bomba, umeme wa majumbani, ujenzi na ushonaji wa mavazi kwa wahitimu 53 waliohitimu mafunzo hayo kwa mafanikio.
Akizungumza katika mahafali yaliyofanyika katika Chuo cha VETA kilichopo kijiji cha Mlezi kata ya Bukanda Mkuu wa wilaya ya Ukerewe Cde, Christopher Ngubiagai amewapongeza wahitimu hao huku akisema ujuzi huo utawasaidia vijana hao kujiajiri na kuwaajiri wengine.
" ... tunawapongeza kwa dhati kwa kuwatambua kwamba ninyi ni fahari ya Tanzania, chuo cha ufundi stadi VETA ni sehemu ya jitihada za serikali kuhakikisha vijana wa kitanzania wanapata ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na kuajiri wengine lakini pia ni sehemu ya kukuza uchumi wetu..." Cde.Ngubiagai.
Akisoma taarifa Mkuu wa chuo hicho Mhandisi Deusdedith Shinzeh amesema miongoni mwa changamoto kubwa zinazowakabili ni ufinyu wa eneo, upungufu wa maji na muamko mdogo wa wanafunzi kujiunga chuoni hapo hasahasa wazawa .
Kwa upande wake mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Ukerewe ambae pia ni Mganga mkuu wa wilaya hiyo Dkt. Charles Mkombe amewasisitiza wazazi na walezi kuendelea kuleta vijana wao katika chuo hicho huku akiahidi kuwa Halmashauri itakuwa bega kwa bega na chuo hicho ili kutatua changamoto zinazojitokeza.
Manyasi Lugembe ni miongoni mwa wazazi wa wahitimu yeye ameeleza kuwa mafunzo ya VETA yamekuwa mkombozi kwa vijana kwa maarifa ya vitendo, na kwamba matokeo wanayoyaona kwa wahitimu yamewafanya wahamasike kwa kusajili watoto wao katika fani hizo.
Anifa Mapesa ni mhitimu wa chuo cha hicho anawapongeza walimu wake kwa kumpa mafunzo mazuri yaliyokuza ujuzi wake katika fani ya uandaaji mavazi huku akisema yupo tayari kufanya kazi na kutengeneza kipato kupitia ujuzi alioupata katika chuo cha VETA Ukerewe.
Akihitimisha kwa kuwatunuku vyeti wahitimu wote Cde.Ngubiagai amewataka wananchi kuendelea kudumisha amani na mshikamano ili kuleta utulivu wa taifa utakaosaidia vijana kusoma kwa amani ili kuzalisha vijana bora watakaokuwa msaada kwa jamii ya Ukerewe na taifa kwa ujumla.
|
|
|
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.