Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Mhe.Ramadhani Salum Mazige ameanza majukumu yake rasmi leo Disemba 05 ,2025 akiwasihi waheshimiwa madiwani kuongeza juhudi zaidi katika usimamizi wa ukusanyaji mapato kwani mapato ndio injini ya uendeshaji wa taasisi nyingi duniani.
Akizungumza wakati wa kikao maalum cha baraza la madiwani la kwanza kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri Mhe.Mazige amesema baraza hilo litajikita zaidi katika masuala ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
"..Muwe na uchungu kwa nini mmekuwepo hapo mlipo, tunapaswa kujenga imani kwa wananchi ,kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa viwango vinavyokubalika ,ni lazima tukusanye mapato ili tufanikishe yote haya.Nawapongeza baraza lililomaliza muda wake wamefanya kazi nzuri.Natamani Halmashauri yetu iende mbele zaidi.."
Kikao hicho kilitanguliwa na waheshimiwa madiwani kuapishwa kiapo cha ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma na cha madiwani.
Aidha Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Cde.Christopher Ngubiagai amewaasa madiwani hao kuwa chachu ya umoja na amani katika maeneo yao.
Nae Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ndugu Vincent Augustino Mbua amewasilisha taarifa ya uwajibikaji wa Halmashauri kwa kipindi chote tangu baraza la madiwani lililopita kuvunjwa (Juni - Oktoba 2025) huku akibainisha kuwa Halmashauri iliweka makisio ya kukusanya na kupokea jumla ya kiasi cha shilingi Bilioni 55,568,650,000.00 kutoka vyanzo mbalimbali.
Angela Matoke ni mkazi wa kata ya Nkilizya anawapongeza madiwani wote na kuwaomba watimize ahadi zao walizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi kwenye mikutano yao ya hadhara.
|
|
|
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.