"... uadilifu ni nguzo ya kuaminika na kufanikiwa walimu wakuu muwajibike kuwajenga walimu na wanafunzi katika masuala ya kusimama imara katika shughuli zao za kila siku kuepuka rushwa katika kusimamia utoaji bora wa elimu, kuzuia utoro na vitendo visivyofaa ili kuleta maendeleo katika jamii..."
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya ya Ukerewe Cde, Christopher Ngubiagai katika mkutano wa tatu wa Umoja wa walimu wakuu wa shule za msingi Tanzania bara (TAPSHA) Ukerewe uliopambwa na kauli mbiu " mtaala ulioboreshwa kwa elimu bora ujuzi na ubunifu kwa maendeleo endelevu ya taifa" uliofanyika katika ukumbi wa Millenium Plaza kata ya Nansio Ukerewe.
Cde.Ngubiagai amewataka walimu hao kuwa wasikivu na wazalendo kutumia vipawa na vipaji vya wale wanaowaongoza huku akiwasisitiza kujitoa kwa ajili ya jamii na kuwalinda na kutengeneza mazingira wezeshi kwa wanafunzi wanaotoka kwenye mazingira magumu.
Akisoma risala katibu Mkuu wa TAPSHA Ukerewe Mwalimu Fadhili Usufu amesema umoja huo umefanikiwa kupunguza idadi ya wanafunzi wasiomudu Kusoma,kuandika na kuhesabu (KKK), usimamizi wa miradi, kutoa msaada kwa wahitaji na kutoa motisha kwa shule zilizofanya vizuri kwa matokeo ya kumaliza elimu ya msingi.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Ukerewe ndugu Vincent Mbua amewasihi walimu hao kushirikiana na wataalam nyakati zote hasa hasa wakati wa kufanya malipo ya miradi na kuwa waangalizi wa miundombinu ya shule huku akikiri kutambua uhaba wa watumishi ndani ya Halmashauri yake ikiwemo sekta ya elimu.
Nae Afisa elimu msingi Mwalimu Bahati Mwaipasi amewapongeza walimu kwa utendaji kazi thabiti uliosaidia kuongeza ufaulu kutoka 82% mwaka 2024 hadi asilimia 87 mwaka 2025 katika mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi huku akisisitiza suala la uchangiaji chakula shuleni kuwa muhimu kwa wanafunzi kufanya vizuri kitaaluma.
Cleophace Majige ni mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kulazu yeye anashauri walimu kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na viongozi ili kuendeleza jitihada za kutengeneza wataalam wazuri watakao litumikia taifa .
Mhe.Ngubiagai amewataka walimu hao kulinda amani, kuishi kwa umoja na mshikamano,kukemea lugha za chuki,dharau na ubaguzi na kuzifanya shule kuwa eneo rafiki la undugu kwa kujenga malezi bora kwa wanafunzi .
|
|
|
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.