Shirika la MAPERECE kwa kushirikiana na AMREF na Hospitali ya Bugando limeendesha mafunzo mahususi kwa mabalozi wa Fistula 37 Wilayani Ukerewe ambapo watoa elimu ngazi ya jamii na watoa tiba za asili lengo la mafunzo ni kuwajengea uwezo mabalozi ili waweze kutimiza majukumu yao katika kuibua wahanga wa Fistula, kuwaelekeza kwenye matibabu na kuwapatia msaada wa kisaikolojia, mafunzo hayo yamefanyika ukumbi wa TAS.
MAPERECE ni shirika lisilo la kiserikali lenye makao yake makuu wilayani Magu. Shirika hili linajihusisha na kutoa huduma kwa wazee, wanawake na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi ili waweze kupata huduma zao za msingi kwenye nyanja za Afya, Haki za binadamu, na kukuza kipato.
Bi. Cecilia Oswago Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya amewataka mabalozi hao kutumia mafunzo hayo ya Ugonjwa wa fistula kutimiza majukumu yao na kuhakikisha lengo la kutoa elimu na kupunguza madhara ya ugonjwa wa fistula ya Uzazi kwa wanawake na kuwaibuwa waadhirika wote na kuwafikisha katika matibabu.
Bw. Revitus John Mratibu Mradi ameeleza kuwa ugonjwa wa fistula ya uzazi unaathari nyingi kwa wanawake ikiwa ni kushuka moyo, kunyanyapaliwa, kutengwa, kukatalia na kujiua. Hivyo amewataka mabalozi walio pata mafunzo hayo kuwafikia wanawake hao na kuwabaini na kuwapa elimu na msaada kisaikolojia itakayowasaidia na kujua kuwa ugonjwa huu unatibika.
Aidha kwa kushirikiana na shirika la AMREF na Hospitali ya Bugando wagonjwa wa Fistula wote wataweza kupata matibabu bila gharama yoyote kwani wafadhili kwa kushirikiana na serikali wamejitoa kuhakikisha ugonjwa unakoma.
Dr. Reolvin Elishaphat ambaye ni mtaalamu wa magonjwa ya Fistula kutoka Hospitali ya Rufaa ya Bugando ameeleza kuwa Fistula ya Uzazi (Obstetric fistula) ni tundu lisilo la Kawaida ambalo halikutakiwa kuwapo kati ya kibofu cha mkojo na njia ya uke (Vesico-Viginal Fistula-VVF) ambapo wanawake wengi hupata VVF, wachache hupata RVF na wachache zaidi hupata zote kwa pamoja.
“Ugonjwa wa Fistula ya Uzazi ni tatizo la nchi zinazoendelea na halipo tena katika nchi zilizoendelea ambapo takribani akina mama milioni 2 wanaishi na fistula duniani, akina mama 50,000 hadi 100,000 wanapata fistula kila mwaka. Inakadiriwa kila mwaka kuna wagonjwa 3,000 wapya wa fistula Tanzania wanatibiwa kwa mwaka ambapo wagonjwa 1600 wanabaki bila matibabu.” Alisema Elishaphat.
Aidha baadhi ya visababishi vya Fistula ya Uzazi ni pamoja na Uchungu pingamizi kwa muda mrefu kabla ya kupata msaada wa kitaalamu unaoleta makazo na kuzuia damu kupita na kasha kusababisha tundu, upasuaji wakati wa uzazi, matibabu kupitia mionzi hasa kwenye matibabu ya magonjwa kama ya Saratani kwenye sehemu ya nyonga na shingo ya kizazi, miundombinu mibovu kupelekea kuchelewa kufika katika vituo vya afya, ucheleweshaji ngazi ya familia na vituo vya afya pamoja na majeraha na magonjwa ya TB ya kibofu cha mkojo.
Dr. Magdalena Dhalla mwakilishi kutoka shirika la AMREF ameelezea dalili za mgonjwa mwenye Fistula ambazo ni kutokwa na haja ndogo au kubwa usiku na mchana bila kujitambua, vidonda sehemu ya siri, harufu mbaya ya mkojo au kinyeesi na kuchechemea kwa sababu ya kuumiza mguu kutokana na uchungu pingamizi.
“Madhara mengine yanayoambatana na ugonjwa wa Fistula ya uzazi ni kupoteza uwezo wa kuzaa tena, kukosekana kwa kushiriki tendo la ndoa, kuporomoka kiuchumi, Hivyo ni vema wagonjwa wakafika hospitali kwa matibabu na ugonjwa huu unatibiwa bure ikiwa ni pamoja na operesheni katika hospitali ya rufaa Bugando au CCBRT iliyoko mkoani Dar es Salaam. ”. Alisema Dr. Dhalla.
Bwana Nombo Anthony na Bi. Vaileth Deus ambao ni mume na mke wakazi wa Nantare kata ya Ngoma ni mashuhuda wa ugonjwa huu, ambapo Vaileth ameeleza kuwa baada ya kujifungua motto wake wa Saba alipatwa na ugonjwa huo ambapo alianza kutokwa na haja bila kujua. “nilichelewa sana kufika hospitali kupata huduma ya kujifungua baada ya kuanza kupata uchungu Lakini baada ya matibabu hospitali ya wilaya nansio nilipewa rufaa na nikaenda Bugando ambapo nilifanyiwa upasuaji na nilikaa huko takribani miezi 8 na niligharamiwa mimi sikutoa kitu mpaka nauli nilipatiwa”. alisema Vaileth.
Nombo ambaye ni mume wa Vaileth ametoa rai kwa wananume kutowatenga wake zao pindi wapatapo maradhi hayo ziaidi wahakikishe wanawafikisha hospitali kwani ugonjwa unatibika.
Crispine Theobald mratibu wa Fistula Ukerewe ameshukuru shirika hilo la MAPERECE kwani kupitia mafunzo hayo wanawake wengi ambao walipoteza matumaini juu ya kutibiwa na kupona ugonjwa wa Fistula kwani sasa wanapokelewa hospitali ya Wilaya na kupewa rufaa kwenda Bugando ambapo gharama zote za matibabu ni bure. “Muondokane na mila potofu juu ya ugonjwa huu kwamba unasababisha na kulogwa la hasha”. Aliongeza Theobald.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.