Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Cde. Christopher E. Ngubiagai ameyataka mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofanya kazi ndani ya Ukerewe kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji na uwazi,kujitolea na mshikamano na jamii,haki na usawa,maadili ya kitaaluma na kijamii sambamba na kuboresha ushirikiano baina yao na serikali.
Akizungumza wakati wa jukwaa la mwaka la mashirika yasiyo ya kiserikali ngazi ya Halmashauri Mhe.Ngubiagai amepongeza takriban mashirika 21 yanayofanya kazi zake za kijamii ndani ya Ukerewe huku akikiri kuona mchango wao mkubwa kwa kuwafikia wananchi ngazi za chini kabisa kwa kuwapatia huduma ambazo serikali peke ake isingeweza kufanikisha kwa haraka.
"..mara nyingi mnafanya kazi ya kuibua changamoto na kuzitafutia suluhisho kuna masuala ya elimu ya afya ya uzazi kwa wasichana, elimu ya mazingira na masuala ya huduma kwa watu wenye mahitaji maalum,kwa kweli mnafanya kazi nzuri sana .."
Akiwasilisha taarifa ya mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofanya kazi zake za kijamii ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Mkuu wa idara ya maendeleo ya jamii amesema katika kipindi cha Januari hadi Machi 2025 jumla ya watu 2,394 wamefikiwa kupitia shughuli mbalimbali za mashirika hayo zinazoendelea kutolewa ndani ya Ukerewe.
Emmerensiana Mkubulo ni mwenyekiti wa shirika la SMAUJATA Wilaya ya Ukerewe yeye ameitaka jamii kuungana katika mapambano dhidi ukatili wa kijinsia huku akina mama kuacha kuwafanyia ukatili waume zao majumbani.
"..Sio wanawake tu wanaofanyiwa ukatili hata kina baba wanakatiliwa sana ni vile wao hawana tabia ya kuzungumza sana,jamii ya Ukerewe embu tubadilike.."
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.