Waziri wa Nchi Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo (MB), amezindua rasmi ujenzi wa majengo mapya katika kituo cha afya Bwisya kilichopo Ukara, ujenzi huo umeanza tarehe 16 Novemba na unatarajia kukamilika baada ya siku 90 na zaidi ya kiasi cha Tsh. 800 Milioni zinatarajiwa kutumika kukamilisha ujenzi huo baada ya kiasi hiko kubaki baada ya maafa na ujenzi unatekelezwa na jeshi kupitia Idara ya SUMA JKT.
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Mhe. Cornel Boniface Magembe amemshukuru Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele katika kipindi cha maafa na kuelekeza rambi rambi zote zilizosalia zitumike katika ujenzi wa kituo hiko. Amemuomba Waziri wa OR-TAMISEMI kuitazama na kuisaidia wilaya ya Ukerewe kwani ina mazingira magumu ya visiwa 38 na zaidi ya visiwa 20 vinakaliwa na watu wanao hitaji huduma muhimu kama matibabu, shule za Bweni ili kuepusha wanafunzi zaidi ya 1200 kuvuka kila siku kuvuka kwenda shule.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella amemshukuru Mhe. Rais kwa kumtuma Waziri na kufika na kuzindua ujenzi wa majengo ili kukamilisha. Amewapongeza wananchi wa Ukara kwa kutoa msaada mkubwa na ni mapenzi ya Mhe. Rais kuwa asilimia 100 ya mafundi vibarua wote watoke Ukara, jambo la msingi ni uadilifu kuanzia kwa wananchi wasiibe vifaa bali wawe walinzi wa vifaa vilivyopo eneo la ujenzi. Kamati ya ujenzi imeundwa na inasimamiwa na kiongozi kutoka Jeshi ambaye ni Luteni Masoudi. “Isitokee kupotea hata msumari mmoja katika ujenzi” alisema Mongella.
Suleimani Said Jafo Waziri wa Nchi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa amewataka SUMA JKT kusimamia kwa umakini na ametoa agizo kuwa kazi ya kukamilisha ujenzi huo iwe imekamilika kufikia tarehe 17 februari 2019 yani siku 90 tu. Dhamira ya Mhe. Rais kuona wananchi wanapata huduma nzuri na yakuridhisha hivyo amewataka watoa huduma wa afya kuhakikisha wanayatumia majengo hayo mapya yatakapo kamilika. Pia amewataka wasimamizi wa vituo vyote vya afya vipya nchi kuwa na smart area yenye mwonekano mzuri wakumridhisha mgonjwa anapokuja kutibiwa.
Jafo Ameeleza kuwa kisiwa cha Irugwa nacho kinahitaji kupata kituo cha afya hivyo amemwagiza Mkurugenzi wa Idara ya Afya TAMISEMI kutafuta fedha ili kufanikisha kupata majengo mapya katika kisiwa hiko. Pia amemwagiza mkurugenzi huyo kutafuta watumishi watakao kuja kufanya kazi maeneo ya visiwani kwani yanakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi.
Jafo amewaasa wananchi wa Ukara kuepukana na mila ya Kutakasana kwani inahatarisha afya zao kuanzia ngazi ya familia hadi taifa, kwani wakiendeleza tamaduni hiyo inaweza kupelekea magonjwa ya kuambukiza kama virusi vya Ukimwi, magonjwa ya homa ya Ini, hivyo amewaasa wale ambao hawajatakaswa wasikubali na watakasaji waache mara moja.
Jafo amezindua ujenzi wa majengo ya wagonjwa wa nje (OPD), jengo la wodi ya wanawake, jengo la wodi ya wanaume, jengo la wodi ya watoto, nyumba 2 za watumishi, jengo la mionzi na jengo la kufulia na kiasi cha Tsh. Milioni 856,122,400/- zilizobaki katika rambirambi baada ya maafa zitatumika katika ujenzi huo.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.