Wilaya ya Ukerewe imepokea Mwenge wa Uhuru leo kutoka Wilaya ya Nyamagana, katika mapokezi hayo wananchi wa Ukerewe wamejitokeza kwa wingi na kuulaki Mwengewa Uhuru mwaka 2019. Katika mbio za Mwenge 2019 katika Wilaya ya Ukerewe umekimbizwa umbali wa KM 77.61 katika kata 4 na umetembelea Miradi 7 yenye thamani ya shilingi 920,819,423.00. Miradi minne (4) imewekewa jiwe la msingi, miwili (2) imezinduliwa na mradi mmoja (1) umetembelewa.
Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa umeweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa vyumba 5 vya madarasa shule ya msingi Chamatuli. Mradi huu ulianza kutekelezwa tarehe 18/12/2018 kwa kujenga vyumba vitano (5) vya madarasa kwa awamu ya kwanza. Ukamilishaji wa ujenzi awamu ya pili ulianza tarehe 1/05/2019 na kukamilika tarehe 14/05/2019. Lengo la mradi ni kupunguza upungufu wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Msingi ya Chamatuli ili kupata mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia. Walengwa wa mradi huu ni wanafunzi 563 watakaotumia vyumba hivi , na walimu wataokuwa wanafundisha.
Mradi umegharimu Tshs 42,521,500.00, kiasi ambacho kimepatikana kutoka kwa Wananchi Tshs 23,242,500.00, Halmashauri Tshs 19,279,000.00.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2019, Mzee Mkongea Ali amefurahishwa namna mradi huo ulivyotekelezwa na amepongeza sana kwani awali shule hiyo ilikua na upungufu mkubwa wa madarasa, hivyo yeye pamoja na msafara wake umeridhia na kuweka jiwe la msingi katika mradi huo.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2019, Mzee Mkongea Ali, ameweka jiwe la msingi katika mradi wa Ujenzi wa jengo la Wagonjwa wa nje katika Zahanati ya Murutunguru ulianza kutekelezwa tangu tarehe 15/01/2018. Mradi huu unahusisha ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje kuanzia hatua ya Msingi.
Lengo la Mradi Kuongeza ufanisi wa utoaji huduma za wagonjwa wa nje kwa kuhakikisha huduma zote muhimu zinatolewa. Wananchi wa eneo la Murutunguru wapatao 15,218 pamoja na wananchi wengine wa maeneo jirani na Kata ya Murutunguru. Itasaidia jamii ya Murutunguru na Wananchi wa maeneo jirani ya Kata kupata huduma za Afya kwa haraka na karibu yao pia kupunguza vifo vya Mama na Mtoto.
Hadi kufikia hatua ambayo mradi upo kwa sasa kiasi cha Tsh. 21,392,560.00 kimetumika kwa mchanganuo ufuatao:- Serikali kuu imechangia Tsh. 650,000.00, Halmashauri imechangia Tsh. 12,744,060.00, Michango ya Jamii Tsh. 7,998,500.00 Mradi huu utagharimu kiasi cha Tsh. 31,670,000.00 hadi kukamilika na kuanza kutumika.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2019, Mzee Mkongea Ali, amezindua Mradi wa hifadhi ya mazingira Shule ya Sekondari ya Bukindo ulianzishwa mwaka 2012, Kufuatia uhitaji wa utunzaji wa mazingira, upatikanaji wa matunda kwa lengo la kuboresha lishe kwa Wananfunzi na kuongeza kipato, tuliomba kuwa na mradi huu kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ambapo tulikubaliwa kupata mradi huu. Miche hii ilitengenezwa kwa njia ya ‘tissue culture’ kwenye bustani ya Shule.
Lengo la Mradi ni Uhitaji wa utunzaji wa mazingira, upatikanaji wa matunda kwa lengo la kuboresha lishe kwa Wanafunzi na kuongeza kipato. Aidha Wanafunzi na Jamii wanapata elimu ya utunzaji wa mazingira kuanzia hatua ya uzalishaji mbegu. Walengwa wa mradi huu ni Wanafunzi na Wananchi wa Tarafa ya Mumlambo na Wilaya ya Ukerewe kwa ujumla.
Mradi huu umegharimu jumla ya Tsh. 5,014,000/=
Malengo ya baadae ya mradi huu ni; kupanda miti ya matunda na mbao kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa mbao kwaajili ya shughuli za ujenzi na matumizi mbalimbali ya Shule, kuongeza mapato ya Shule na upatikanaji wa kuni na kumarisha hali ya Lishe Shuleni.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2019, Mzee Mkongea Ali, ameweka jiwe la msingi katika mradi huu wa maji Murutunguru ulioanza kutekelezwa tarehe 15/4/2019, baada ya kuongezeka kwa mahitaji ya maji katika kijiji cha Murutunguru, Halamashauri imechukua uamzi wa kufanya ujenzi wa mradi huu kwa kujenga vituo vya kuchotea maji 5 kwa thamani ya Tshs 9,110,680.00 kwa fedha za Serikali kuu Tshs. 4,249,180.00 na Halmashauri Tshs. 4,681,500.00. Hata hivyo vituo 10 zaidi vitajengwa ili kufanikisha jumla ya vituo 15 katika vitongoji vyote vilivyopo kwenye kijiji cha Murutunguru.
Kazi kubwa zilizofanyika katika upanuzi wa mradi huu wa maji ni:-
Ulazaji wa bomba lenye ukubwa wa inchi 1.5 zenye umbali wa km 1.6
Ujenzi wa vituo 5 vya kuchotea maji.
Lengo la Mradi Kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa kijiji cha Murutunguru na vitongoji vyake. Wananchi zaidi ya 1,500 wa vitongoji vya karibu na Center katika kijiji cha Murutunguru watanufaika na mradi huu. Katika kuendeleza mradi huu Halmashauri imeunda chombo cha kusimamia uendeshaji na kukipa elimu ili kiweze kuhamasisha wananchi kutunza, kulinda mradi na miundombinu yake.
Ujenzi wa Mradi huu umegharimu kiasi cha Tshs 9,110,680.00.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2019, Mzee Mkongea Ali, amepongeza mradi huu na ametaka kuendelezwa kujengwa na kukamilika hatimae uendelee kutoa huduma kwa Wananchi wafurahie huduma ya maji kupatikana chini ya kauli mbiu isemayo “Maji ni haki ya kila mtu, tutunze vyanzo vyake na tukumbuke kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa”.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2019, Mzee Mkongea Ali, Kiwanda hiki kilianza kutekelezwa tangu tarehe 01/07/2016 na shughuli zinaendelea kama ilivyopangwa. Shughuli hizo ni;- Ujenzi wa banda, Kununua na kusimika mashine za kusaga na kukoboa mahindi.
Lengo la Mradi Kukuza viwanda ndani ya nchi, Kuboresha na kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa Wilayani Ukerewe. Hii ni pamoja na kuboresha kiwango cha ajira kutokana na shughuri zinazofanyika katika kiwanda hiki hiki.
Walengwa ni Kaya 1397 za wananchi wa bugorola pamoja na wananchi wengine wa ndani na nje ya Wilaya. Manufaa yake Kukuza uchumi ndani ya wilaya kwa kuongeza ajira za muda na za kudumu, Kupata elimu juu ya uzalishaji na usindikaji wa mazao ya chakula, Kusaidia kupambana na njaa, kuongeza usalama wa chakula na kuimarisha lishe katika Wilaya.
Mradi huu umegharimu jumla ya Tsh 244,000,000/= kwa mchanganuo ufuatao; fedha ambazo zimetolewa na Mwekezaji mwenyewe ambaye ni Mtanzania ni Tsh. 144,000,000.00 na Wahisani Tsh. 1,000,000.00.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2019, Mzee Mkongea Ali, ameweka jiwe la msingi katika mradi huu na amempongeza muwekezaji huyo kwani anatimiza adhma ya serikali kuwa ni nchi ya viwanda.
Mradi wa ujenzi wa daraja la Kilimabuye na matengenezo ya barabara ya Kakerege – Namagondo Km 7.86. umetekelezwa na Wakala wa barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Mwanza na kusimamiwa na Ofisi ya Meneja wa TARURA Wilaya ya Ukerewe, kazi ilianza tarehe 10/04/2018 na kukamilika 23/08/2018.
Mradi huu unalenga kuboresha miundombinu ya barabara ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Ukerewe, Wananchi wote waliopo katika Kata 2 za; Kakerege na Namagondo zenye Vijiji 4 vya Kakerege, Kilimabuye, Mukituntu na Namagondo wapatao 16,257.
Mradi wa ujenzi wa daraja hili la vipimo vya urefu wa mita 16.2 upana mita 8 kina mita 3 na matengenezo ya barabara Km.7-86 umetekelezwa kwa fedha za miradi ya maendeleo kutoka katika Mfuko wa barabara (ROADS FUND) za mwaka wa fedha 2017/2018 kwa gharama ya kiasi cha Tsh. 459,685,691.90.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2019, Mzee Mkongea Ali, amezindua barabara hiyo na daraja hilo na amepongeza TARURA kwa kuhakikisha ubora unazingatiwa na kuzidisha viwango kwani daraja ni zuri sana.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2019, Mzee Mkongea Ali,ametembelea mradi wa Kusambaza Maji Bukindo/Kagunguli ulianza kutekelezwa 9/3/2017 na kukamilika 30/8/2018 na kuzinduliwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018. Mradi unahudumia Wananchi kutoka vijiji viwili vya Bukindo na Kagunguli vyenye wakazi wanaokadiriwa kuwa 5,000 ndani ya kijiji cha Bukindo na Kagunguli. Wananchi wametoa ushirikiano mkubwa katika mradi huu kwa kutoa maeneo ya kujenga tenki ya kuhifadhi maji, na kibanda cha mitambo ya kusukuma maji (Pump house).
Mradi huu umejengwa kwa lengo la kuboresha afya ya wananchi kwa kuwapatia huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama katika umbali wa karibu wa mita 400 kulingana na sera ya maji ya Taifa ya mwaka 2002.
Mradi huu umejengwa kwa kutumia fedha za ndani toka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia mfuko wake wa Uwekezaji katika Sekta ya Maji. Mradi huu umegharimu jumla ya Tsh 139,096,992.00 fedha ambazo zimetolewa na Serikali kuu.
Kimeundwa chombo cha kusimamia uendeshaji wa Mradi, Jumuiya ya watumiaji maji Bukindo-Kagunguli ambacho kilipewa mafunzo na kuwajengea uwezo wa kusimamia mradi tangu Juni 2018. Aidha hadi sasa, Jumuiya ya watumiaji maji imeweza kuunganisha wateja binafsi 53.
Mradi huu umejengwa chini ya usimamizi wa MWAUWASA na unaendeshwa kwa ushirikiano kati ya Jumuiya ya Watumiaji Maji na Ofisi ya Mhandisi wa Maji wa Wilaya wa Ukerewe.
Pia Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2019, Mzee Mkongea Ali ameteketeza nyavu na zana mbalimbali haramu za uvuvi 413 zilizokamatwa kwa kipindi cha mwenzi Machi 2019 hadi mei 2019, ambazo ni kokoro,timba, nyavu za dagaana nyavu za makila zote zikiwa na thamani ya thamani ya tsh 209,986,000.00. zana hizo haramu za uvuvi zimechomwa katika eneo la Bukongo mtoni. Amewataka wananchi wa Ukerewe kuachana na uvuvi wa kutumia zana haramu na kufuata utaratibu, kanuni na sheria.
Katika kupokea taarifa mtambuka Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2019, Mzee Mkongea Ali, amepokea taarifa mbalimbali za kisekta ambapo amewataka wananchi wa Ukerewe na visiwa vyake kujitahidi kuachana na matumizi ya madawa ya kulevywa, kujilinda dhidi ya maambukizi ya virusi vya ukimwi, kuachana na rushwa.
Aidha Katika hatua nyingine Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2019, Mzee Mkongea Ali, ametoa fedha tsh. 10,000,000.00 ikiwa ni mikopo ya vikundi mbalimbali ili vikundi hivyo kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi. Na ameshiriki kujionea namna wanavyofanya shughuli zao.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.