Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Ndugu Vincent Augustino Mbua amefanya kikao na wasimamizi wa huduma za afya ngazi ya msingi inayojumuisha waganga wafawidhi,makatibu wa afya,wafamasia,wauguzi wafawidhi, maafisa lishe, maafisa ustawi na wataalam wa maabara kwa lengo la kujitambulisha kwao, kukumbushana maadili ya kazi, kujadili changamoto zinazoikabili idara hiyo sambamba na kutengeneza mlengo wa pamoja katika masuala ya ukusanyaji mapato.
".. Mapato ni kila kitu katika taasisi,tunawajibika kukusanya ili tuweze kujiendesha.Nasisitiza matumizi ya mifumo tuliyonayo na kufunga kamera kwenye baadhi ya maeneo sensitive.."Amesema
Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa upo ushahidi wa ongezeko la mapato kwa kasi katika vituo vya kutolea huduma za afya vinavyotumia mfumo wa GoTHomis na maeneo yaliyofungwa CCTV camera.
Aidha amewataka wataalam hao kutoa huduma bora kwa wateja ikiwa ni sehemu ya maadili ya kazi yao na kuwavutia wateja wao kujitokeza kwa wingi vituoni kupata huduma za afya huku akiwasihi kuanza kujiponya wao wenyewe afya za akili zao na baadae kusaidia wengine.
Nae Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt.Charles Mkombe amesema ofisi yake imeandaa utaratibu wa kutoa pongezi kulingana na utendaji kazi wa wataalam wa afya vituoni kwa wote watakaofanya vizuri na watakaofanya vibaya lengo ikiwa ni kuweka hamasa ya ukusanyaji mapato na kuboresha huduma za afya zinazotolewa.
Afisa utumishi Charity Mbirity amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa kufuata maadili na kanuni za taaluma yao ya afya na kuwataka waache kujichukulia sheria mkononi kwenye masuala ya matibabu ya msamaha bila kufuata taratibu za kazi.
Akihitimisha kikao hicho Mkurugenzi Mbua amewataka wataalam hao kuachana na tabia zisizofaa kama ulevi uliokithiri huku akiwatia moyo kuendelea kufanya vizuri wakati changamoto zao zikiendelea kutatuliwa .
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.