Wadau wa maji Wilayani Ukerewe wamefanya mkutano ulio andaliwa na EWURA pamoja na NAUWASA kwa ajili ya Taftishi juu ya maombi ya kurekebisha bei za huduma ya majisafi yanayotolewa na mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Nansio (NAUWASA), Taftishi imefanyika katika ukumbi mkubwa wa Halmashauri ambapo umehusisha wadau mbalimbali ikiwemo baraza la ushauri la watumiaji huduma ya maji na mwakilishi wa ofisi ya Waziri Mkuu na umehudhuriwa na Mkurugenzi Mhandisi Musira Nyirabu pamoja na mmoja wa wajumbe wa bodi ya EWURA Ahmad S.K Kilima, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Mhe Estominh F. Chang’ah ambaye alikua mgeni rasmi, na kaimu Mkurugenzi Mtendaji (W) Moses Nduligu.
Mamlaka ya Majisafi na usafi wa mazingira mjini Nansio (NAUWASA) ilianzishwa Julai 1,2007 na ilikua na wajibu wa kuhakikisha wananchi wanapata majisafi na salama. Hadi sasa mradi umefanikiwa kujenga mradi mkubwa wa majisafi na usafi wa mazingira uliokamilika mwezi Juni,2016. Mradi ulihusisha ujenzi wa chanzo cha maji na kituo cha kisasa cha tiba Nebuye, ujenzi wa matenki 2 yakiwa na uwezo wa kuhifadhi lita za ujazo 3,350,000.00 kwa pamoja, na mabomba ya usambazaji maji jumla ya kilomita 52.8 na kufanya uzalishaji wa maji kuongezeka kutoka lita 7,000 hadi kufikia 2,500,000 kwa siku.
Changamoto zinazoikabili NAUWASA ni pamoja na gharama kubwa za umeme wa kuazalisha, kutibu na kusukuma maji kwa wateja ambazo zimefikia wastani wa Tsh.18.3 kwa mwezi, gharama hizi ni zaidi ya 96% ya mapato yote ya mamlaka kwa mwezi.
NAUWASA inapendekeza ongezeko la bei kwa wastani wa asilimia 266.50.
EWURA ina jukumu la kudhibiti na kusimamia watoa huduma katika sekta ya majisafi na usafi wa mazingira(ikiwa ni pamoja na sekta ya nishati) pamoja na kudhibiti ubora wa huduma inayotolewa na uhalalo wa bei ya huduma husika.
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Mhe. Estominh Francis Chang’ah amefungua mkutano huo na amewataka wadau kuelewa umuhimu wa huduma ya maji na kuchangia maoini yao ili kuleta maboresho katika huduma inayotolewa na NAUWASA.
Wananchi mbalimbali ambao ndio wadau wakuu wa maji wametoa maoni yao mbalimbali ikiwa ni pamoja na NAUWASA ihakikishe inadhibiti na kuzuia upotevu wa maji hasa mabomba yanayovuja, kuongeza miundombinu na kusajili wateja wapya na kupunguza ukatikaji wa maji.
Mhandisi Goodluck Mmari Katibu Mkuu kutoka Baraza la ushauri la watumiaji wa huduma zinazodhibitiwa na EWURA (EWURA CCC) ametoa maoni mengi baadhi ni pamoja na NAUWASA kuongeza ufanisi wa kiutendaji hii inaenda pamoja na kuongeza masaa ya kutoa hudua kwa siku kufikia masaa 24 tofauti na masaa 12 ya sasa, uwiano wa wateja waliofungiwa dira kiwango cha sasa ni 88% badala ya 100%. Kuondolewa kwa kundi la wateja wasio na mita (unmetered customers) hivyo kusahauri wateja wote wawekewe dira pia wameshauri MWAUWASA kuongeza nguvu kazi kwa kuwa na watumishi wakutosha kulinganisha na sasa ambao 9 wameanzimwa kwa Mkurugenzi Mtendaji(W) na 3 wa MWAUWASA.
Ezamo Sawaki Maponde Mkurugenzi msaidizi kutoka ofisi wa Waziri Mkuu pia amekua na maoni kuwa ongezeko hilo la bei kwa sasa halifai na itakapobidi kuongezwa basi iwe ni hatua kwa hatua, hii inatokana na kuwa chanzo cha maji kipo nan i chanzo cha kudumu NAUWASA ina miundombinu ya kisasa sana lakini 15% tu ya wakazi wa Ukerewe ndio wanapata maji hivyo kunahaja ya kujikita zaidi katika kuimarisha huduma na kuongeza wateja kwa kasi.
NAUWASA imetakiwa kuandika maelezo kwa kina juu ya huduma inayotoa na namna gani wataanza kufanyia kazi mapendekezo na maoni yote yaliyotolewa na wadau wa maji Ukerewe, mabaraza mawili na EWURA ndio majibu yaatarudishwa kulingana na uchambuzi zaidi.
Mmoja wa mkazi wa Ukerewe akitoa maoni katika mkutano wa wadau wa maji
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.