Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella amewataka watendaji wote wanaohusika katika ukamilishaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Ukerewe ikamilishwe kwa wakati ili kuanza kuwahudumia wananchi. Ameyasema hayo katika ziara yake ya kikazi katika Wilaya ya Ukerewe kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za Serikali.
Ziara ya imekua na lengo la kukagua na kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika idara tofauti tofauti na wakati wa ziara ya Mhe. John Mongella ametembelea amekagua miradi katika sekta za elimu, afya na maji.
Mongella ameelekeza kwa Idara ya Elimu sekondari kuhakikisha kuwa shule ya sekondari Nyamanga iliyopo katika Tarafa ya Ukara kata ya Nyamanga inakamilisha usajili mapema iwezekanavyo. Amewataka pia kusimamia na kukamilisha ujenzi wa shule hiyo ambayo ilipata Milioni 12.5 ili kukamilsha miundombinu. Mpaka sasa shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 226 ambapo wasichana 109 na wavulana 117. Ameyasema hayo wakati wa kuweka jiwe la msingi katika shule hiyo ambayo itasaidia wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda sekondari ya Bwisya na Bukiko.
Akiwa kisiwani Ukara Mongella ametembelea kituo cha afya Bwisya ambapo kuna ujenzi wa kituo hiko. Kituo cha Afya Bwisya kilipata fedha takribani Milioni 800 fedha za rambimrambi zilizobaki wakati wa maafa ya MV. Nyerere na Mhe. Dkt. John Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliagiza fedha hizo zitumike kujenga kituo hiko. Ujenzi huo mpaka sasa upo katika hatua ya ukamilishaji majengo hayo yanajengwa na SUMA JKT.
Mongella ametembelea na kukagua ujenzi wa kituo cha afya Muriti unaojengwa kwa gharama ya milioni 400 zilizotolewa na serikali. Amewataka kukamilisha ujenzi huo kufikia tarehe 1 juni mwaka huu.
Katika hatua nyingine Mhe. John Mongella Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ametembelea kata ya Murutunguru na kukagua ujenzi wa chuo cha ualimu Murutngu ambao upo kwenye hatua ya ukamilishaji amewataka kuendelea kusimamia ubora. Amekagua pia zahanati ya Murutunguru ambayo bado ipo hatua ya renta amehimiza jitihada ziongezwe ili kukamilisha zahanati hiyo.
Mongella amepongeza hatua ya halmashauri katika Idara ya Maji kusimamia na kuhakikisha Murutunguru na kagunguli wanapata maji safi na salama kutoka kwenye chanzo cha maji Bukindo. Amewataka wananchi kutunza na kulinda vyanzo vya maji ilividumu miaka mingi ili kuendelea kuwahudumia.
Amepata fursa ya kuzungumza na wananchi wa maeneo ya Bwisya na Nyamanga, ambapo amewataka kuendelea kushirikiana na serikali katika kuhakikisha jamii inapata maendeleo kwa ukaribu na wakati.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.