Katibu tawala wa Wilaya ya Ukerewe Ndugu Alan Augustine Mhina akimwakilisha Mkuu Wilaya ya Ukerewe ameongozana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo kufanya ziara kukagua miradi inayotekelezwa kupitia fedha za mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF).
Akizungumza akiwa katika mradi wa ujenzi wa nyumba ya mtumishi wa afya "2 in 1" uliogharimu kiasi cha shilingi milioni 92 fedha zilizotolewa na programu ya kupunguza umaskini (TPRPIV) chini ya ya ufadhili wa nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi OPEC uliopo kata ya Igalla kijiji cha Bwasa Mhina amewataka wataalam kuendelea kusimamia miradi yote kwa uadilifu na kuhakikisha inakuwa ya viwango vinavyokubalika.
".. hongereni mradi ni mzuri mkumbuke hizi ni fedha za serikali kwa manufaa ya wananchi, muendelee kutelekeza kwa uadilifu mkubwa mkiwashirikisha wananchi wenyewe kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa mradi.." amesema Mhina
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo mratibu wa TASAF Wilaya ya Ukerewe Bi. Jenita Damaseni amesema mradi huo upo hatua za ukamilishaji huku akitaja manufaa ya mradi huo kuwa ni pamoja na kupata maji safi na salama kwani mradi tayari una mfumo wa kuvuna maji ya mvua lita 10,000 kutoka katika matenki mawili yenye ujazo wa lita 5000 kila moja sambamba na upatikanaji wa mazingira bora ya kuishi watumishi wa afya kaya 2 ambao wanaishi mbali na eneo la kazi.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Ndugu Vincent Augustino Mbua amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa fedha nyingi za miradi ya maendeleo anazoendelea kuzielekeza ndani ya Wilaya ya Ukerewe.
"..tuna kila sababu ya kumuunga mkono Rais wetu kwa jitihada kubwa anazofanya za kuleta mabadiliko chanya katika sekta mbalimbali.."
Ihoelo Bandiho ni mkazi wa kijiji cha Bwasa yeye anaipongeza serikali kwa kuboresha mazingira ya watumishi wa afya kijijini kwao huku akikiri huduma za afya kuboreshwa kutokana na uwepo wa daktari .
Mhina amehitimisha ziara hiyo katika mradi wa ujenzi wa zahanati katika kijiji cha Kakerege kata ya Kakerege uliopatiwa kiasi cha shilingi milioni 92.41 ambao upo hatua ya kupiga lipu
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.