Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (MB) Naibu Waziri wa Afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto. Akiwa na wataalamu wa wizara ya afya, pamoja na mganga mkuu wa mkoa, amefanya ziara wilayani Ukerewe kwa lengo la kukagua huduma zinazotolewa katika vituo vya afya na hospitali ya wilaya, ambapo ametembelea hospitali ya wilaya ya Ukerewe, vituo vya afya vya Nakatunguru na Kagunguli.
Mganga Mkuu wa Wilaya Dkt. Joshua S. Monge ameeleza kuwa mpaka kufikia 2017/2018 kuna jumla ya zahanati 28 za serikali zinafanya kazi na halmashauri imejipanga kufungua zahanati zingine mbili(2) na hii ni katika kutekeleza sera yetu ya kusogeza huduma za afya kwa wananchi. Halmashauri kwa kushirikiana na wananchi imetenga bajeti kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa zahanati katika vijiji vya Buguza, Bukindo, Mibungo, na Nabweko na ujenzi wa nyumba za watumishi katika zahanati za Buguza, Busunda, Nabweko, Bukindo na Mibungo.
Monge ameeleza kuwa upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi katika vituo umeimarika hadi kufikia asilimia 92% katika kipindi cha mwaka 2018. Huduma za afya katika wilaya inakabiliwa na upungufu wa watumishi kwa takribani 76%,kukosekana kwa jengo/kitengo maalumu kwa ajili ya utoaji wa huduma kwa wagonjwa mahututi, upungufu wa stand by genereta, alisema Monge.
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Mhe. Estomihn Chang’ah akimkaribisha Mhe. Naibu Waziri amemweleza jiografia ya wilaya kuwa ni ya visiwa hivyo kunauhitaji wa kuangaliwa kwa jicho la tofauti ilikuweza kuwasogezea huduma ya afya watu waishio maeneo ya visiwani.
Mhe. Joseph Mkundi Mbunge wa jimbo la Ukerewe ameshukuru serikali kwa fedha ilizoleta katika kuboresha miundombinu ya afya ambapo kituo cha afya Bwisya kilipata milioni 400 na ujenzi upo hatua za mwisho na kituo cha afya Muriti kimepokea Tsh. 400,000,000 kwa ajili ya ujenzi/ukarabati ambapo taratibu za awali za ujenzi wa mradi huo tayari zimeanza. Pia kulingana na hali ya kijiografia ya kisiwa chetu cha Ukerewe kunahaja ya kuwa na boti ya wagonjwa wa dharura (ambulance boat) itakayohudumia wagonjwa wadharura tuu kuwapeleka hospitali ya wilaya au mwanza ambapo kuna hospitali kubwa zaidi. Alisema Mkundi.
Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (MB) Naibu Waziri wa Afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto akizungumza katika ziara hiyo amepongeza uongozi wa halmashauri na wilaya kwa kuwa na mpangilio mzuri, usafi na utoaji mzuri huduma katika hospitali ya wilaya na vituo vya afya kwani malalamiko yamepungua kwa kiasi kikubwa.
Ndugulile amefanya ziara hii wilayani Ukerewe baada ya Mbuge wa Ukerewe Mhe. Mkundi kuwasilisha bungeni hali ya huduma ya afya na changamoto ya kijiografia ya kisiwa kuwa na changamoto nyingi. Akitoa majibu ya changamoto zinazoikabili halmashauri katika sekta ya afya ameahidi kushughulikia suala la upatikanaji wa vifaa vitakvyowezesha kufunguliwa na kuanzishwa kwa huduma ya wodi ya wagonjwa mahututi, huduma ambayo hivi sasa haipo na ni huduma muhimu kwa wananchi wa kisiwa cha Ukerewe. Hivyo amewataka kutenga jengo litakalotumika kwa wagonjwa mahututi. Pia ameahidi kushughulikia suala la upatikanaji wa watumishi wa afya kwani itasaidia kuondoa upungufu unaoikabili hospitalinya Wilaya, vituo vya afya na zahanati.
Ndugulile amewataka usimamizi ufanyike kwa ukaribu katika maeneo ambayo serikali imetoa fedha kwa ajili ya kuwasogezea huduma wananchi na kuwa lengo hilo limefikiwa.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.