Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Joseph Magufuli amefanya ziara ya kikazi ya siku moja wilayani Ukerewe ambapo amefanya shughuli kadhaa ikiwemo uzinduzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Nebuye, na jiwe la msingi upanuzi wa chuo cha Ualimu Murutunguru.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt John Magufuli amezindua Mradi wa Maji Mjini Nansio uliotekelezwa kupitia mpango wa uboreshaji wa huduma za Majisafi na Usafi wa Mazingira ya Ziwa Viktoria, mradi huu unatekelezwa katika nchi tano za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo ni Burundi, Kenya, Tanzania, Uganda na Rwanda, ambapo kila nchi mradi unatekelezwa katika miji mitatu na kwa Tanzania ni Sengerema, Geita na Nansio. Nansio mradi umekamilika. Mradi umegharimu kiasi cha Tsh. Bilioni 10.9. Alisema Mhe. Prof. Makame Mbarawa (MB).
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt John Magufuli Leo ameweka jiwe la msingi kwa ajili ya upanuzi wa Chuo Cha Ualimu Murutunguru, “chuo Cha Murutunguru kwa sasa walimu wanaohitimu ni ngazi ya cheti, lengo la serikali ni kianze kutoa ngazi ya Diploma na baadae kikiongezewa miundombinu kiweze kutoa shahada.” Alisema Magufuli.
Rais Magufuli amewapongeza Viongozi wa Wizara ya Elimu kwa kusimamia vizuri miradi inayotekelezwa na Wizara hiyo, amewashukuru washirika wa Maendeleo hususan nchi ya Uingereza kwa kuendelea kufadhili miradi ya Elimu. Upanuzi wa ujenzi wa Chuo hicho unahusisha jengo la Utawala, vyumba vya madarasa, bwalo la Chakula, hosteli za wanafunzi, jengo maalumu la kupokelea umeme na ujenzi wa mifumo ya Maji na umeme. Ujenzi huo utagharimu takriban bilioni mbili nukta Tatu na inatarajia kukamilika oktoba mwaka huu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amefanya mkutano wa hadhara katika uwanja wa Ukuta Mmoja ambapo ameeleza namna ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano inavyotekeleza majukumu yake katika kuboresha maisha ya watanzania. Amewataka wananchi kuachana na uvuvi haramu na kutumia zana sahihi na amemtaka Waziri Luaga Mpina Waziri wa Mifugo na Uvuvi kuendelea kupambana na wale wasiotaka kufanya uvuvi usio wa tija katika ziwa Viktoria.
Rais Magufuli amesema Serikali itajenga barabara ya kutoka Rugezi kwenda Nansio yenye urefu wa zaidi ya Km 12 kwa kiwango cha lami. “ ukerewe siwezi kuisahau” alisema Rais Magufuli. Aidha ameahidi kusaidia mchakato wa uanzishwaji wa kiwanda cha samaki ili wavuvi wanufaike na uvuvi wao katika ziwa Viktoria.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.