Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John mongella amefanya ziara ya siku moja katika Wilaya ya Ukerewe ambapo aliambatana na wataalamu mbalimbali wa ngazi ya Mkoa na kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo. Katika ziara hiyo alipokelewa na Mkuu wa Wilaya Estomihn Chang’ah na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Moses Nduligu.
Mongella ametembelea na kukagua shule mbili za Sekondari za Bukongo na Pius Msekwa ambazo zilipata fedha za serikali (P4R) kupitia wizara ya Elimu, sayansi na Teknolojia kujenga mabweni mawili kila shule, madarasa manne kila shule ambapo mradi huo una gharimu zaidi ya Tsh. 500,000,000/-.
Mongella amezitaka shule hizo kufanya marekebisho kama walivyoshauriwa ili miundombinu hiyo iweze kuwa ya manufaa zaidi kwa wanafunzi na kwa muda mrefu zaidi. Ujenzi umefika katika hatua nzuri ambapo mpaka sasa ni marekebisho madogo ndiyo yamesalia, mabweni hayo yatanufaisha wanafunzi wanaoishi mbali na shule pia wanafunzi wa kike kuwaondolea changamoto za njiani pindi wajapo shule na kutoka.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella ametembelea soko la samaki katika eneo la Kakukuru lilojengwa na LVEMP ambapo litanufaisha wafanyabiashara wa samaki katika eneo kubwa la kakukuru na visiwa jirani na kuwezesha urahisi wa kazi na biashara katika eneo hilo.
Pia alipata fursa ya kutembelea shule ya sekondari ya wasichana kagunguli katika kata ya Kagunguli ambapo alikutana na uongozi wa shule na wanafunzi hao ambapo walibainisha changamoto walizonazo kama maji na ujenzi wa bwalo la chakula na Mhe. Mkuu wa Mkoa John Mongella akawaondoa hofu kuwa mradi wa maji Bukindo unaojengwa na MWAUWASA ukikamilika utaondoa kero hiyo na kuhusu bwalo aliahidi kurudi wakati mwingine ili kuendesha Harambee ilikukamilisha ujenzi huo.
Akiwa katika Hospitali ya Wilaya Mongella amekabidhi mashuka 80 yatakayotumika hospitalini na kusaidia kupunguza changamoto ya mashuka. Amewataka mashuka hayo yatumike na sio kuwekwa stoo na Halmashauri waandae mkakati bora kuhamasishwa watu kujiunga na bima ya afya kwani kwa 10000 tu watu wa kaya wapatao kumi wanaweza kuhudumiwa. Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Dr. Mohamed Kilolile ameeleza nia ya kusaidia mashuka hayo kwa Hospitali ya wilaya ni kuisaidia ili iweze kuhudumia wananchi kwani kwa wilaya ndio kama hospitali ya rufaa hivyo hawanabudi kuisaidia. Pia Mkuu wa mkoa amezindua na kukabidhi vitambulisho kwa watoto waliosajiliwa katika huduma ya TOTO AFYA CARD kwa watoto chini ya miaka 18.
Mongella amehitimisha ziara yake katika ukumbi wa Halmashauri kwa kukabidhi mabati kwa wahanga wa upepo mkali ulioleta uharibifu wa nyumba na mali katika kata ya Igalla. Pia amekutana na waendesha pikipiki wa Ukerewe na kuwasihihi vyama viwili vya bodaboda vilivyopo hapa Ukerewe kuungana na kuwa na chama kimoja ilikuweza kuwahudumia wanachama wao vizuri, pia amewataka bodaboda kutii sheria za barabarani na kuagiza SUMATRA kushirikiana na nao na kuwapatia mafunzo ya wiki mbili ilikupunguza ajali za barabarani.
Copyright ©2022 Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe . All rights reserved.